Merkel akutana na Papandreou wa Ugiriki | Magazetini | DW | 27.09.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Merkel akutana na Papandreou wa Ugiriki

Suala lililochukua nafasi ya juu katika uhariri katika magazeti ya Ujerumani leo ni kuhusu mkutano kati ya kansela wa Ujerumani Angela Maerkel na waziri mkuu wa Ugiriki, George Papandreou.

default

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (CDU) akiwa na waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou mjini Berlin

Suala lililochukua nafasi ya juu katika uhariri katika magazeti ya Ujerumani leo ni kuhusu mkutano kati ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa Ugiriki, Papandreou. Pia kuna suala la kuwataka Wapalestina kurejea katika meza ya mazungumzo pamoja na Israel, na mjadala kuhusu uchangiaji wa viungo vya mwili hapa Ujerumani.

Likizungumzia kuhusu mkutano kati ya Ugiriki na Ujerumani, gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung, linaandika.

Wagiriki wanafahamu hali ngumu ya kutawaliwa na mataifa ya kigeni. Kibonzo kilichochapishwa katika gazeti moja nchini Ugiriki kuhusu Merkel kinaweza kufungamanishwa na kikao hiki ambacho kina hali ya wasi wasi mkubwa wa Ugiriki kuongozwa kama watoto. Wasi wasi huu unajipenyeza sio tu kwa wale wanaofahamu uwezo mkubwa wa Ujerumani. Katika hili inakuja hali ya mbinyo , kwamba serikali ya George Papandreou iko mwishoni mwa uwezo wake, na nchi hiyo ina hatari kubwa ya kuangukia katika hali ya ombwe la uongozi.

Katika mada hiyo hiyo gazeti la Badische Neueste Nachrichten linalochapishwa mjini Karlsruhe linaandika:

Kansela anaweza katika baadhi ya nyakati katika mikutano yake ya kimkoa akashangazwa hata na msimamo wake binafsi , kwamba kwa muda mrefu hakuna kitu maalum kinachotokea katika eneo hili na pia kuhusu msimamo wake wa mapenzi katika masuala ya kimsingi. Hadi sasa suala hili la madeni ya Ugiriki limekuwa likijadiliwa chini chini katika vyama vya kisiasa tu nchini Ujerumani , kukiwa na mawazo tofauti kuhusu msaada kwa Ugiriki.

Gazeti la Der neue Tag linazungumzia kuhusu hatua za kuleta amani katika mashariki ya kati. Linaandika.

Mwishowe rais wa Marekani anaweza kulazimika kutumia kura ya turufu . Lakini ni Obama huyu huyu ambaye mwaka mmoja uliopita akishangiriwa sana katika kikao cha baraza kuu la umoja wa mataifa , alisema kuwa ana matumaini kuwa mwaka mmoja ujao atalikaribisha taifa jipya huru la Palestina katika umoja wa mataifa. Gazeti linadokeza kuwa katika ulimwengu wa mataifa ya Kiarabu Marekani na umoja wa Ulaya unaathirika na hali ya kutoaminika.

Obama UN

Rais wa Marekani Barack Obama akizungumza katika baraza kuu la umoja wa mataifa

Gazeti la Leipziger Volkszeitung linajadili kuhusu mjadala wa kuchangia viungo vya mwili hapa Ujerumani. Gazeti linaandika.

Serikali bado inaendelea kuliona suala hili kuwa ni la kujitolea binafsi. Lakini mpango wa waziri wa afya wa sheria ya upatikanaji wa viungo vya kuokoa maisha unaleta mbinyo kidogo wa ulazima, na hii ni sawa kabisa. Suali ni kuwa watu wengi zaidi wawe tayari kujitolea, kutoa kiungo ambacho kinaweza kuokoa maisha ya mwingine, kwa kuwa na kitambulisho maalum. Hii inaeleweka, linasema gazeti hilo, lakini nani anataka kucheza na kifo? Na yule anayeamua kufanya operesheni ya kuchangia kiungo ni lazima apate muda wa kuizowea hali hiyo.

Naam hayo ndio tuliyoweza kuwakusanyia katika udondozi wa magazeti ya Ujerumani.

Mwandishi : Sekione Kitojo / Inlandspresse

Mhariri : Othman Miraji

 • Tarehe 27.09.2011
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12h68
 • Tarehe 27.09.2011
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12h68