1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT: Majeshi yaendelea kukabiliana na wanamgambo wa Kiislamu, Lebanon.

24 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CByv

Msemaji wa kijeshi wa Lebanon amesema meli ya kijeshi ya nchi hiyo imezishambulia na kuzizamisha mashua mbili zilizokuwa zikibeba wanamgambo wa kundi la Fatah al-Islam waliokuwa wakikimbia kutoka kambi ya wakimbizi ya Nahr al-Barid.

Hapo awali serikali hiyo iliwataka wanamgambo wa kiislamu waliojificha katika kambi hiyo ya wakimbizi wa kipalestina kaskazini mwa nchi hiyo wajisalimishe au waendelee kukabiliwa kijeshi.

Waziri wa ulinzi wa nchi hiyo , Elias Murr alisema majeshi yake kamwe hayatashauriana na wanamgambo wa kundi la Fatah al-Islam.

Majeshi hayo yamekuwa yakipambana na wanamgambo hao tangu siku ya Jumapili iliyopita.

Maelfu ya watu wamearifiwa kukimbia kambi hiyo ya Nahr al-Barid na kwa mujibu wa wakazi wa kambi hiyo, baadhi ya maiti zimezikwa kwenye vifusi.

Kiasi wapalestina laki nne wanaishi katika kambi za wakimbizi nchini humo. Kulingana na mwafaka wa mwaka 1969 wa mataifa ya Kiarabu, majeshi ya Lubanaan hayaruhusiwi kuingia kwenye kambi za wakimbizi wa Kipalestina.