1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Baraza la UN halijaafikiana juu ya Palestina

Tatu Karema
12 Aprili 2024

Kamati ya Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa imeshindwa kuafikiana kuhusu jibu la pamoja juu ya ombi jipya la kutaka uanachama kamili wa Mamlaka ya Palestina katika Umoja wa Mataifa

https://p.dw.com/p/4egpD
Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya kura ya azimio la Gaza linalotaka kusitishwa mara moja kwa mashambulizi iliofanyika mjini New York Marekani mnamo Machi 25,2024
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: Andrew Kelly/REUTERS

Baada ya mkutano uliofanyika Alhamisi mjini New York nchini Marekani, balozi wa Malta katika Umoja wa Mataifa Vanessa Frazier ambaye kwasasa ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo ya Baraza la Usalama, alisema kuwa theluthi mbili ya mataifa wanachama wa baraza hilo yaliunga mkono ombi hilo laPalestinala kutaka hadhi ya uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa huku matano yakipinga.

Frazier amesema kuwa atasambaza ripoti kuhusu suala hilo miongoni mwa wanachama wa Baraza la Usalama haraka iwezekanavyo.

Soma pia: Palestina yataka uanachama kamili ndani ya Umoja wa Mataifa

Kamati hiyo inaonekana kutokuwa na uwezekano wa kupendekeza kura ya hoja hiyo katika Baraza la Usalama . Hata hivyo, taifa lolote mwanachama linaweza kuwasilisha azimio sawa na hilo wakati wowote.

Kulingana na duru za kidiplomasia, Algeria inapanga kufanya hivyo katika wiki zijazo.

China inaunga mkono ombi la Palestina 

China  inaunga mkono unachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa. Wakati wa mkutano na waandishi habari hapo jana mjini Beijing, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa nchi Mao Ning alisema kuwa mzozo unaoendelea kati ya Palestina na Israel na mzozo mkubwa wa kibinadamu uliosababisha ni ukumbusho mwingine kwamba njia pekee ya kumaliza mzunguko mbaya wa migogoro ya Palestina na Israeli ni kutekeleza kikamilifu suluhisho la mataifa mawili, kuanzisha taifa huru la Palestina na kurekebisha dhuluma ya kihistoria ya muda mrefu kwa Wapalestina.

Ning ameongeza kuwa China inaunga mkono uanachama kamili wa Umoja wa Mataifa kwa Palestina na inaunga mkono hatua za haraka za Baraza hilo kufanikisha hilo.

Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi akihudhuria mkutano wa waandishi habari mjini Beijing mnamo Machi 7,2024
Waziri wa mambo ya nje wa China Wang YiPicha: Wang Zhao/AFP

Kwa hoja hiyo ya Palestina kufanikiwa, angalau wanachama tisa wa Baraza la Usalama watapaswa kuiunga mkono na kutopingwa na mwanachama yoyote wa kudumu katika baraza hilo kama vile China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani.

Blinken aitaka China kuizuia Iran kutoishambulia Israel

Wakati wa mazungumzo kwa njia ya simu kati ya waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi na mwenzake wa Marekani Antony Blinken, Blinken aliitaka China kutumia ushawishi wake kuizuia Iran kutoishambulia Israel. Haya ni kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Soma pia: Kiongozi mkuu wa Iran aapa kulipiza kisasi dhidi ya Israel

Hii ni baada ya kuongezeka kwa wasiwasi wa mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka Iran baada ya shambulizi la Israel dhidi ya ubalozi wake mdogo mjini Damascus nchini Syria mnamo Aprili 1.

China yalaani shambulizi la Israel dhidi ya ubalozi wa Iran nchini Syria

Wang ameeleza ghadhabu ya China juu ya shambulizi hilo huku akisisitiza kuhusu haki isiyoweza kukiukwa ya usalama wa taasisi za kidiplomasia na haja ya kuheshimu uhuru wa Iran na Syria.

Vikosi ya Israel vyawauwa Wapalestina wawili

Vikosi vya Israel vimewaua kwa kuwapiga risasi Wapalestina wawili katika uvamizi uliofanyika mapema leo karibu na mji wa Tubas katika eneo la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu. Haya yameripotiwa na shirika la habari laPalestina Wafa.

Jeshi la Israel halikutoa tamko la haraka kuhusu shambulizi hilo.

afp,dpa