1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Zuma si mfano wa utawala bora"

Maja Dreyer20 Desemba 2007

Suala moja linalozungumziwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii ni kuteuliwa kwa Jacob Zuma kama kiongozi mpya wa chama cha ANC cha Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/CeLB
Jacob Zuma
Jacob ZumaPicha: AP

Jingine ni mpango wa Umoja wa Ulaya kuongeza bei za magari makubwa kutokana na kochi mpya kwa ajali ya ulinzi wa hali ya hewa. Tuanze basi na uchaguzi katika chama cha ANC na maoni ya mhariri wa “Süddeutsche Zeitung” kuhusu kuteuliwa kwa Jacob Zuma:


“Kiongozi huyu mpya wa chama cha ANC alitumia makosa ya mtangulizi wake Mbeki. Kushindwa kwa Mbeki kuzigusa nyoyo za watu kulimsaidia Zuma kushinda. Lakini ikiwa kweli Zuma atachaguliwa kuwa rais atakabiliwa na kazi ngumu. Kwani itabidi atafute maamuzi. Maskini wanataka ajira, chakula na mustakabali bora. Na tena maskini hawana subira. Bado Zuma hajasema atatatua vipi matatizo haya. Badala yake aliwatuliza wawekezaji na viongozi wa uchumi kwamba si lazima kubadilisha sera za chama cha ANC. Lakini maana yake ni kwamba hali itabakia hiyo hiyo. Hata wafuasi wa Zuma hawatayavumilia haya.”


Mhariri wa “Berliner Zeitung” pia ana wasiwasi kuhusu sera za Jacob Zuma. Ameandika:


“Katika majuma yaliyopita, Jacob Zuma alijaribu kuwashawishi wafanyibiashara kwamba hana mpango wa kutekeleza mageuzi. Lakini ndiyo haya wapigaji kura wake wanayoyataka. Lete bunduki yangu, waliimba kwenye mkutano mkuu wa ANC. Kweli, Zuma si mfano wa utawala bora. Namna alivyowatolea mwito wafuasi wake waandamane dhidi ya kesi ya rushwa na ubakaji zilizosikilizwa mahakamani na hivyo kuishurutisha mahakama si ishara kwamba Zuma anafaa kwa kiti cha urais. Sasa anajionyesha kama mtu asiye na msimamo mkali. Lakini tabia yake ya kutumia mamlaka vibaya na kutojali taasisi za kiserikali itaimarisha mifumo ya serikali ambayo imeshayaathiri mataifa mengi ya Afrika.”


Kwa mada ya pili tunaelekea hapa Ulaya ambapo halmashauri ya Umoja wa Ulaya ilizusha mjadala mkali. Kulingana na mswada mpya, wanunuzi wa magari yasiyo madogo wanatakiwa kulipa Euro elfu moja zaidi kama mchango kwa ulinzi wa hali ya hewa. Kuhusu mada hiyo gazeti la “Kölner Stadt-Anzeiger” linauliza:

“Kwa nini mswada huu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya unaolenga kupunguza utoaji wa gesi chafu kupitia magari ulizusha hasira nyingi? Hususan makampuni ya Ujerumani yanayotengeneza magari kama Mercedes, Audi na BMW yanalaumu kwamba yataathirika zaidi na wanasema soko litabadilika. Pia kansela Angela Merkel na waziri wa mazingira wanakubali kwamba sera ya utunzaji wa hali ya hewa inatumiwa na nchi kama Ufaransa na Italy kutekeleza sera zao za kiuchumi kwa gharama ya Ujerumani.”


Gazeti la “Frankfurter Neue Presse” linakosoa vikali malalamiko ya wanasiasa na wanauchumi hapa na pale likikumbusha kwamba:


“Kwenye mkutano wa Bali kuhusu hali ya hewa, nchi za Ulaya zimetokeza kama mfano mzuri katika sera hizo - kinyume na Marekani, China au India - zinapigania sana kuzuia kuongezeka kwa joto duniani. Lakini siku tatu baada kurudi kutoka Bali, siasa imerudi kwenye hali ya kawaida. Wafaransa, Waitalia na Wajerumani wanagombana juu ya jinsi ya kutekeleza utunzaji wa hali ya hewa. Hukuna anayetaka kujitolea. Ugomvi huu kuhusu bei za magari ni mfano. Na migogoro itazidi, kwani utunzaji wa hali ya hewa una gharama zake.”