1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma ahimiza mabadiliko Zimbabwe

16 Agosti 2012

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amekutana na viongozi wa Zimbabwe na kuwataka kuafikiana juu ya mchakato wa mageuzi ya kisiasa kuepusha vurugu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika katika kipindi cha mwaka mmoja.

https://p.dw.com/p/15qUW
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma
Rais wa Afrika Kusini Jacob ZumaPicha: picture-alliance/dpa

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Harare baada ya mazungumzo na Rais Robert Mugabe na pia waziri mkuu Morgan Tsvangirai, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema kuna maendeleo yaliyofikiwa kuelekea kwenye muafaka juu ya katiba mpya, ingawa bado kuna vizingiti viichache vinavyosalia.

Kupunguzwa kwa mamlaka ya rais

Rais Robert Mugabe na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai, mahasimu wanaoshiriki madaraka
Rais Robert Mugabe na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai, mahasimu wanaoshiriki madarakaPicha: AP

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema chama cha Rais Robert Mugabe, ZANU-PF ambacho kilisukumwa kwenye makubaliano ya kushiriki madaraka na chama cha waziri mkuu Morgan Tsvangirai, kitafanya kila kinachoweza kuchelewesha makubaliano juu ya katiba mpya.

Mwandishi wa Detsche Welle nchini Zimbabwe Columbus Mavhunga anasema ZANU-PF inahofia katiba mpya itapunguza mamlaka ya rais Robert Mugabe.

''Kitu muhimu kwa ZANU-PF ni kwamba kwa sasa kinashikilia madaraka zaidi, na hii ndio sababu chama hicho hakitaki kuridhia mabadiliko katika katiba, ambayo yanalipa bunge mamlaka zaidi na kupunguza nguvu za rais. Hii ni hali ambayo haikuzoeleka tangu Zimbabwe ilipopata uhuru wake kutoka kwa waingereza mwaka 1980.'' Amesema Mavhunga.

SADC, jumuiya yenye mizozo mingi

Rais Zuma ambaye ni mpatanishi katika mzozo wa Zimbabwe hata hivyo, amesema kuwa ameshuhudia hatua iliyopigwa kwenda mbele, na kwamba vikwazo vilivyopo sasa siyo vikubwa kama ilivyokuwa siku za nyuma. Zuma alisema atatoa ripoti juu ya maendeleo hayo kwenye mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, ambao utafanyika kesho katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo.

Mkutano huo wa Maputo utayaiangazia mizozo mingine ya kisiasa na kiuchumi inayozikumba nchi wanachama, mkubwa zaidi ukiwa ule wa kisiwani Madagascar. Jumuiya ya SADC inawashinikiza wahusika katika mzozo huo, rais wa sasa Andry Rajoelina na mtangulizi wake Marc Ravalomanana kufuata mchakato utakaoielekeza nchi yao kwenye uchaguzi.

Kikwazo kikubwa katika mchakato huo ni kwamba Rajoelina hataki Ravalomanana agombee katika uchaguzi ujao, akimhusisha na mauaji ya watu 36 walioshiriki katika maandamano yaliyouangusha utawala wake.

SADC pia ni mdhamini wa mpango wa kisiasa uliofanikishwa kuundwa kwa serikali ya umoja wa taifa mwaka 2008, na itataka kura ya maoni ifanyike juu ya katiba mpya itakayowezesha kufanyika uchaguzi ambao utahitimisha utawala wa kipindi cha mpito.

Uchaguzi na vita

Titel: MPLA eröffnet Wahlkampf in Angola - Anhänger der Regierungspartei Schlagworte: Wahlen, Wahl 2012, Angola, Politik, Wahlkampf, MPLA, Regierungspartei Ort: Viana, Luanda, Angola Fotograf: Quintiliano dos Santos Datum: 31.07.2012 Beschreibung: Anhänger der Regierungspartei MPLA am 31. Juli in Viana (Großraum Luanda). Hier eröffnete die MPLA ihren offiziellen Wahlkampf für die Parlamentswahlen am 31. August 2012.
MPLA eröffnet Wahlkampf in Angola - Anhänger der RegierungsparteiPicha: Quintiliano dos Santos

Masuala mengine yatakayozungumziwa kwenye mkutano huo ni uchaguzi mkuu nchini Angola mwishoni mwa mwezi huu, ambao ni wa pili tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hata hivyo watetezi wa haki za binadamu wanasema mazingira nchini humo yanatatiza uwazi katika uchaguzi huo.

Mgogoro mwingine kwenye meza ya mazungumzo ya viongozi wa Jumuiya ya SADC, ni mapigano mapya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kati ya jeshi la serikali na waasi wa M23. Watu takribani laki mbili na nusu wameyaacha makazi yao kwa kuyakimbia mapigano hayo.

Wachambuzi wanaamini kuwa Jumuiya hiyo ya ushirikiano wa itaujadili mzozo huo, lakini jukumu la kuutatua litabakia mikononi mwa nchi za kanda ya Afrika Mashariki.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman