1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya kwanza ya waziri wa ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika

Miraji Othman7 Januari 2010

Ujerumani na ushirikiano wa kimaendeleo katika Rwanda, Kongo na Msumbiji

https://p.dw.com/p/LODb
Waziri wa Ujerumani wa ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, Dirk NiebelPicha: AP

Ziara ya kwanza ya waziri wa ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel, inaelekea Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Msumbiji. Hii ni ziara ya nchi zinazotafautiana. Na hivyo ndivyo ilivofikiriwa. Dirk Niebel amezichagua nchi hizo tatu shirika ambazo ni tafauti katika mtizamo wa ushirikiano katika maendeleo. Miradi ya Ujerumani ya ushirikiano katika maendeleo katika nchi hizo inasambaa katika sekta mbali mbali, kutoka elimu, hifadhi endelevu ya mali asili hadi miradi ya afya au utoaji mikopo.

Rwanda inaonekana kuwa ni mfano mzuri, angalau linapokuja suala la nia ya serekali katika siasa ya maendeleo. Ilivokuwa haina rasil mali na ina ongezeko kubwa la wakaazi, nchi hiyo ndogo, yenye waakazi milioni tisa katika Afrika Mashariki, inawekea uzito katika maendeleo ya kiufundi, inataka kuwa Singapore ya Afrika, kituo cha huduma katika Kusini Mashariki ya Afrika. Wahakiki wanazungumza kwamba Rwanda, wakati huo huo, imekuwa nchi ya kidikteta inayoendelea- haki za kiraia na uhuru wa vyombo vya habari ni mambo yalio macheche. Bila ya kujali yale yanayoondoshwa na ambayo hayaambatani na ile fikra ya mustakbali utakaokuwa na maajabu ya kiuchumi unaonawiri. Lakini, kwa upande mwengine, nchi gani ya Kiafrika, isiokuwa Rwanda, inayoweza kutoa ushahidi wa maendeleo wazi yaliopatikana katika sekta za elimu au kupungua vifo vya watoto wadogo? Hamna. Rwanda yaonesha iko njiani kuweza, kiuchumi, kusimama kwa miguu yake, hivyo inakaribiana na mawazo ya waziri Dirk Niebel linapokuja suala la ushirikiano wa kimaendeleo ulio na malengo.

" Mimi ninazungumza juu ya ushirikiano wa maendeleo ambao utafanya uwawezeshe washirika wetu wa maedneleo wasihaitaji tena misaada ya nje, lakini waweze wenyewe kujitegemea, wenye umuhimu sawa katika ushirikiano na madola mengine."

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inatimiza masharti yote ya kuweza kujikamatia mikononi mwake yenyewe maendeleo yake, lakini kunakosekana nia ya kisiasa. Kutoka Kigali, waziri huyo wa ushirikinao wa kiuchumi na maendeleo wa Ujerumani atakwenda mashariki ya nchi ya Kongo yenye mali nyingi za asili. Kongo imeonesha kwamba chaguzi huru peke yake sio dhamana kwamba kufanikiwa kujengwa demokrasia. Kwa siasa ya kigeni na ushirikiano wa maendeleo ya Ujerumani, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ni ukurasa mgumu. Jeshi la Ujerumani mwaka 2006 lilihakikisha kwamba kunafanyika uchaguzi wa kwanza wa kidemokarsia katika nchi hiyo ilio na wakaazi milioni 60, lakini, hata hivyo, vita vimekuwa vikiendelea mashariki ya nchi hiyo. Si mambo mengi yaliobadilika tangu mwaka 2007 pale mtangulizi wa waziri Dirk Niebel alipotangaza kwamba Ujerumani itaendeela kuisaidia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo katika kukiuka hali ya matumizi ya nguvu na kuijenga upya nchi hiyo.

Sio tu na Umoja wa Mataifa, ambapo waziri huyo wa ushirikiano wa maendeleo wa Ujerumani atakutana na wawakilishi wake, lakini linazuka suala: na nani mtu atashirikina naye huko Kongo? Ripoti ya Umoja wa Mataifa ilihakikisha hapo mwezi Novemba kwamba jeshi la Kongo lilishiriki katika biashara ya silaha. Jumuiya huru, kama vile Human Rights Watch, ziliripoti juu ya kuuliwa raia katika Kivu ya Kaskazini, mauaji yaliofanywa na wanajeshi wa serekali. Kwa muda mrefu pande zinazozozana hazitafautiani kutokana na sababu za kisiasa au kinadharia. Ushirikiano na mafungamano kila siku yanafungwa upwa huko Mashariki ya Kongo. Hivyo, waziri Niebel atakusudia kukutana na jumuiya za kiraia na waathirika wa vitendo vya matumizi ya nguvu. Atatembelea hospitali ambako wanawake waliobakwa wanahudumiwa na pia atapata picha juu ya hali ya wakimbizi ambao kwa miaka wemehama njumba zao kwa hofu ya waasi na jeshi la serekali...

Msumbiji ni nchi ya mwisho katika ziara hii ya waziri Niebel. Msumbiji inatoa sura ya mchanganyiko. Wahakikia wanahofia kurejea kwa dola ya chama kimoja, bado kunakosekana ugawaji ulio sawa wa maendeleo na miundo mbinu, kunakosekana siasa iliofaulu ya kupeleka maendeleo mashambani, licha ya kwamba sio Ujerumani tu, lakini nchi nyingi fadhili, kwa miaka, zimegharimia zaidi ya nusu ya bajeti ya nchi hiyo. Waziri huyo mpya wa ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ataiangalia hali hiyo kwa jiocho la uhakiki, kwani yeye mwenyewe hivi karibuni aliweka wazi kwamba wizara yake sio idara ya misaada ya jamii kwa dunia, lakini inataka kutumia kwa uangalifu fedha za walipa kodi kwa ajili ya malengo ya siasa za maendeleo. Waziri huyo wa Ujerumani katika nchi hizo tatu atapata mwangaza mwingi , lakini pia vivuli.

Mwandishi:Ute Shaeffer

Mfasiri:Othman Miraji

Mhariri:Aboubakary Liongo