Zapatero akataa kukutana na Kagame
17 Julai 2010Waziri Mkuu wa Hispania amekataa kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa pamoja na Rais wa Rwanda Paul Kagame mjini Madrid baada ya upinzani kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu. Waziri Mkuu Jose Luis Rodriguez Zapatero alitarajiwa kukutana na Kagame pamoja na katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon kwa ajili ya kikao cha kundi la watetezi wa malengo ya maendeleo ya milenia. Lakini vyama vya upinzani pamoja na makundi ya haki za binadamu yalimtaka Zapatero kutohudhuria kwa sababu ya kesi zilizoko mahakamani nchini Hispania dhidi ya maafisa 40 wa Rwanda wanaohusishwa na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Waziri wa mambo ya kigeni Miguel Angel Moratinos alichukua nafasi ya Waziri Mkuu Zapatero, na mkutano huo ulihamishwa kutoka makao rasmi ya serikali na kufanyika katika hoteli mjini Madrid.