1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa kupambana na ongezeko la joto duniani

P.Martin2 Aprili 2007

Maafisa wa ngazi ya juu katika Umoja wa Ulaya hii leo wamezihimiza Marekani,China na India kuimarisha juhudi za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani.Vile vile wameapa kuzisaidia nchi zinazoendelea kupambana na ongezeko la joto duniani.

https://p.dw.com/p/CHH0

Mjini Brussels,kamishna wa mazingira wa Umoja wa Ulaya,Stavros Dimas alipofungua mkutano wa juma moja wa wataalamu wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani,aliikosoa Marekani kuwa inajiburura kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Akasema,kitendo hicho kinachelewesha kupata makubaliano ya kimataifa ya kuhusu hatua za dharura zinazohitaji kuchukuliwa,ili kuzuia ongezeko la joto duniani.

Dima,ameihimiza Marekani kutia saini mkataba wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, akisema kuwa ni muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kuwa na msimamo mmoja,ili hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa kupambana na ongezeko la joto duniani.Australia pia imekosolewa kuwa haina dhamira ya kisiasa kuidhinisha Itifaki ya Kyoto inayotoa wito wa kupunguza gesi zinazochafua mazingira.

Wakati huo huo waziri mkuu wa Ubeligiji Guy Verhofstadt,ametoa wito kwa Marekani,China na India zijiunge na mataifa mengine kuchukua hatua zaidi,kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa. Amesema,ni shida kujiepusha na hatua zisizovutia, lakini hata hivyo ni wajibu wa wanasiasa wa nchi zote duniani,kuchukua hatua zilizo ngumu.

Itakumbukwa kuwa mwezi uliopita,viongozi wa Umoja wa Ulaya walikubaliana kupunguza gesi ya kaboni dayoksaidi inayochafua mazingira na badala yake wamesema zitumie zaidi,nishati endelevu.

Msimamo huo wa Umoja wa Ulaya,ni msingi wa majadiliano mapya ya mkataba mpya wa kimataifa, kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa,ambao mwaka 2012 unatazamiwa kuchukua nafasi ya Itifaki ya Kyoto ya hivi sasa.

Nchi za Umoja wa Ulaya zinatoa asilimia 14 ya gesi zinazochafua mazingira,na Marekani ambayo ni mchafuzi mkubwa kabisa wa mazingira duniani,hutoa kama asilimia 25.

Siku ya Ijumaa,katika mkutano wa mjini Brussels, jopo linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa, linatazamia kukamilisha ripoti inayoeleza vipi ongezeko la joto duniani huathiri maisha ya binadamu.Vile vile ripoti hiyo inatarajiwa kueleza kuwa nchi masikini duniani zilizotoa sehemu ndogo sana ya gesi zinazochafua mazingira,ndio zitakazoathirika vibaya zaidi kutokana na ongezeko la joto duniani.