1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WIESBADEN : Putin akutana na Merkel

15 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Ff

Rais Vladimir Putin wa Urusi na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wameanza mazungumzo ya siku mbili katika mji wa magharibi wa Ujerumani wa Weisbaden

Mazungumzo hayo yalichelewa kuanza kuliko vile yalivyokuwa yamepangwa baada ya ndege ya rais Putin kuchelewa kuondoka kutokana na hali mbaya ya hewa mjini Msocow. Mazungumzo yao yanatarajiwa kulenga juu ya biashara na uhusiano wa nchi mbili hizo.Pia wanatazamuwa kugusia masuala wanayohitilafiana kati ya mataifa ya magharibi na serikali ya Urusi kama vile mpango wa nuklea wa Iran na hatima ya jimbo la Serbia la Kosovo.

Urusi inapinga kuongezwa kwa vikwazo dhidi ya Iran vilivyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pia inasisitiza kwamba madai ya Serbia ya kutaka jimbo lililojitenga la Kosovo lisipewe uhuru yanapaswa kutiliwa maanani.

Kabla ya kuondoka Moscow Putin alielezwa juu ya njama ya kumuuwa wakati wa ziara yake iliopangwa kufanyika wiki hii nchini Iran.

Shirika la habari la serikali la Interfax limetaja duru katika idara za ujasusi nchini Urusi zikisema kwamba washambuliaji wa kujitolea muhanga wamepatiwa mafunzo kufanya mauaji hayo.

Wizara ya mambo ya nje ya Iran imetupilia mbali tishio hilo kuwa halina msingi kabisa.