1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIndonesia

Waziri Mkuu wa China ahutubia mkutano wa ASEAN

6 Septemba 2023

Viongozi wa mataifa ya kusini mashariki mwa Asia wanakutana na wenzao wa Marekani, China, Japan na nchi nyingine washirika ikiwa ni sehemu ya mkutano wa kilele wa jumuiya ya kanda hiyo, ASEAN.

https://p.dw.com/p/4W0M5
Mkutano wa ASEAN, Jakarta, Indonesia
Waziri Mkuu wa China, Li Qiang (kushoto) akilakiwa na Rais Joko Widodo wa Indonesia wakati akiwasili kwenye ukumbini kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya ASEAN, unaofanyika Jakarta.Picha: MAST IRHAM/REUTERS

Viongozi wa Jumuiya hiyo wanaitumia siku ya pili ya mkutano huo wa mjini Jakarta, Indonesia kufanya mazungumzo na wenzao kutoka madola yenye nguvu na yale yenye usuhuba wa karibu na kanda ya kusini mashariki mwa Asia.

Ni jadi kwa Jumuiya ya ASEAN kuwaalika viongozi wa Marekani, China, Japan na Korea Kusini kushiriki mkutano wao wa kilele wa kila mwaka. Mara hii India, Australia na Canada pia zimealikwa.

Suala la usalama wa eneo la Pasifiki, kitisho cha nyuklia kwenye rasi ya Korea, kutanuka ubavu wa China kijeshi na njia bora za kuutatua mzozo wa kisiasa wa Myanmar ni mada zuilizowashughulisha viongozi wa ASEAN tangu mkutano huo ulipofunguliwa hapo jana.

China yatoa mwito wa kuepukwa "vita vipya baridi"

Mapema hii leo kundi la viongozi ASEAN lilikuwa na mkutano wake na China - taifa jirani lenye nguvu za kiuchumi na linalojitanua kijeshi - ambalo limekuwa ajenda ya juu ya mjadala kwenye kanda hiyo ya Asia na bahari ya Pasifiki.

Waziri Mkuu wa China, Li Qiang
Waziri Mkuu wa China, Li Qiang Picha: Yasuyoshi Chiba/REUTERS

Waziri Mkuu wa China Li Qiang ndiyo ameongoza ujumbe wa Beijing kwenye mkutano huo na ametumia hotuba yake kuelezea umuhimu wa kuepusha kile amekitaja kuwa "vita vingine baridi" katika kushughulikia mizozo baina ya mataifa ulimwenguni.

Li amesema ni lazima nchi duniani zijifunze "kumaliza tofauti na kutatua migogoro kwa njia za kiungwana"

Wawakilishi wa Japan na Korea Kusini nao walikuwemo ukumbuni wakati Li akihutubia na viongozi wa mataifa hayo nao walitoa hotuba baadae.

Matamshi ya kiongozi huyo wa China yumkini yalinuwia kuikumbusha kanda ya ASEAN kutochagua upande katikati mwa kizungumkuti cha sera za kutunishinia misuli baina ya Marekani na China zinazowania ushawishi miongoni mwa mataifa 10 yanayounda jumuiya hiyo.

Marekani kusisitiza demokrasia na uungaji mkono kwa kanda ya ASEAN

Indonesia ASEAN
Mkutano wa ASEAN unaofanya Jakarta, Indonesia Picha: Mast Irham/AP Photo/picture alliance

Wakati Qiang tayari amewasilisha mtizamo wa China, Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris naye anafanya mkutano na viongozi wa ASEAN mchana huu.

Maafisa wa Washington wamesema Kamala atasisitiza dhamira ya Marekani ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na Jumuiya ya ASEAN na kanda nzima ya Bahari ya Hindi na Pasifiki.

Tayari kiongozi huyo amegusia suala jingine tete linaloikabili Jumuiya hiyo. Nalo ni mzozo wa kisiasa nchini Myanmar ambapo amesema Marekani inaendelea kuhimiza demokrasia kama suluhu kwa kizaazaa kinachoshuhudiwa kwenye taifa hilo tangu jeshi lilipochukua madaraka mwaka 2021.

Kesho Alhamisi (07.09.2023) kutakuwa na mkutano mwengine wa kilele wa mataifa ya Asia mashariki ambao utahudhuriwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov.

Mkutano huo kwa kawaida ni jukwaa pana kushinda lile la Jumuiya ya ASEAN na hujadili masuala makubwa ya kisiasa na misuguano kwenye eneo la Asia Mashariki. Lavrov tayari yuko mjini Jakarta kumwakilisha rais Vladimir Putin.