1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watuhumiwa kuwa na njama za kuiba watoto wa Afrika!

30 Oktoba 2007

Watu 18 wanakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuwateka nyara watoto zaidi ya mia moja nchini Chad ili kuwapeleka barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/C7fx

Mashtaka hayo yanawakabili wafanyakazi 9 wa shirika la misaada kutoka Ufaransa, wandishi habari , wahudumu 7 wa ndege kutoka Uhispania na wananchi wawili wa Chad.

Watu hao walikamatwa nchini Chad mapema wiki jana walipokuwa wanajitayarisha kuondoka nchini pamoja na watoto hao.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amelaani kitendo hicho kuwa haramu na kisichokubalika.

Akizungumza akiwa na ghadhabu , rais Idriss Deby wa Chad ameuliza iwapo watu hao walikuwa na nia ya kuwauza watoto hao kwa waharibifu ama walikuwa na nia ya kuwaua ili watoe viungo vya miili yao na kuviuza?

Lakini shirika la misaada la Ufaransa linalohusika na mkasa huo limekanusha madai kwamba lilikuwa na nia ya kuwateka nyara watoto hao.

Msemaji wa shirika hilo ameeleza kuwa shirika lake liliamini, watoto hao ni yatima kutoka Darfur magharibi mwa Sudan.

Lakini madai ya shirika hilo yamekanushwa na watumishi wa shirika la watoto la Umoja Mataifa UNICEF waliosema kuwa ,watoto hao ambao sasa wamewekwa kwenye nyumba ya yatima katika mji wa Abeche nchini Chad wanaangusha vilio usiku kuwalilia wazazi wao na wamesema wanatoka kwenye vijiji vya Chad.

Shirika la misaada la Ufaransa Zoe’s Ark limedai lilikuwa na nia ya kuokoa maisha ya yatima 103 kutoka Darfur na kuwapeleka nchini Ufaransa ambapo walikuwa wanasubiriwa na familia zilizokuwa tayari kuwalea.