1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 40 wauawa na wengine 141 kujeruhiwa katika mlipuko Afghanistan

Kalyango Siraj7 Julai 2008

Serikali yadai hao ni waTaliban

https://p.dw.com/p/EXeC
Polisi ya Afghanistan ikiwa mahali pa tukio la shambulio la kujitoa mhanga katika ubalozi wa India mjini Kabul, jumatatu, Julai 07, 2008.Picha: AP

Takriban watu 40 wameuawa na wengine 141 kujeruhiwa katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga katika ubalozi wa India mjini Kabul Afghanistan.

Ingawa hakuna kundi ambalo limejigamba kuhusika na shambulio hilo lakini kundi la Taliban ndio linanyoshewa kidole.

Mtu ambae amejitolea mhanga ameendesha gari ambalo lilikuwa na baruti na kuligonga katika milango ya ubalozi wa India nchini Afghanistan.Gari hilo limeipuka na,kwa mujibu wa maofisa, limewauwa watu zaidi ya 40 mkiwemo raia wanne wa India.Wengi wa waliouawa ni raia wa kawaida.

Wengine zaidi ya 141 wamejeruhiwa.

Miili ya watu ilitapakaa kote mahali pa tukio hilo.Mlipuko huo umetokea wakati watu walikuwa wanasubiri kupata visa kwenda India katika ubalozi huo.

India ni mshirika mkubwa wa Afghanistan.Utawala wa Kabul unaendesha mapambano makali dhidi ya Wataliban.

Hili ndilo mojawapo wa shambulio kubwa kufanywa mjini Kabul tangu utawala wa Wataliban uondolewe madarakani na uvamizi ulioongozwa na Marekani wa mwaka 2001.Shambulio lingine lilitokea Aprili 27 wakati wapiganaji walipomfyatulia risasi rais Hamid Karzai alipokuwa anahutubia taifa.

Wengi wanahisi shambulio hilo limefanywa na wataliban.Lakini kundi hilo limekanusha kuhusika.Msemaji wake Zabihullah Mujahid ameliambia shirika la habari la AFP kuwa kundi lake halijahusika kamwe .

Balozi wa India,Jayan Prasad,ambae hakujeruhiwa katika shambulio hilo,amevihakikishia vyombo vya habari kuwa raia wanne wa India ni miongoni mwa watu waliofariki.

Nayo wizara ya mashauri ya kigeni ya India,imesema kuwa wanajeshi wake wawili waliokuwa wanalinda ubalozi huo waliuawa katika shambulio hilo ambalo wizara ya mambo ya ndani ya Afghanistan inasema ni shambulio la kigaidi.

Duru za kuaminika zinasema kuwa miongoni mwa raia wanne wa India walifariki na watumishi wa ubalozi huo ni mwanadiplomasia mmoja pamoja na muambata wa kijeshi.

Shambulio hilo limelaaniwa na Ikulu ya Marekani pamoja serikali ya India.

Katika taarifa iliotolewa mjini New Delhi,serikali ya India imesema kuwa visa vya kigaidi kama hicho kamwe havitaizuia kukamilisha azma yake kwa serikali na watu wa Afghanistan.

India inadhamini miradi mbalimbali nchini Afghanistan.

Shambulio la leo jumatatu limekuja baada ya maafisa wa Afghanistan kusema jumapili kuwa kombora la majeshi ya ushirika limewauwa takriban watu 23 waliokuwa wanakwenda kuhudhuria harusi mashariki mwa Afghanistan.

Shambulio hilo lilitokea katika mkoa wa Nangarhar na wananchi wa kawaida wamesema wale waliouawa katika shambulio hilo walikuwa watoto pamoja na wanawake.

Marekani imekanusha madai hayo.