1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watatu wafungwa Ujerumani kwa ugaidi

6 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CXiF

DÜSSELDORF.Mahakama ya jimbo la North Rhine-Westphalia nchini Ujerumani imetoa hukumu ya kufungwa kwa watu watatu wanaotuhumiwa kuwa wafuasi wa kundi la al Qaeda, baada ya miezi 18 ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Katika hukumu hiyo, mtuhumiwa mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka saba, mwengine sita na wa tatu miaka mitatu na nusu.

Watuhumiwa hao ambao wana asili ya Syria na Palestina walipatikana na makosa ya kusaidia mtandao wa kigaidi pamoja na udangayifu katika bima ili kupata fedha za kufadhili shughuli za al Qaeda.

Nchini Marekani mahakama kuu ya nchi hiyo jana ilianza kusikiliza kesi iwapo wafungwa katika gereza la Guantanamo Bay Cuba wako chini ya katiba ya Marekani.

Mawakili wa wafungwa hao walihoji kuwa wateja wao wamekuwa wakinyimwa kimakosa haki ya kutaka mahakama isikilize malalamiko ya sababu za wao kuwekwa kizuizini.

Wafungwa hao wanashikiliwa katika gereza hilo kwa makosa ya kuhusika na ugaidi na Marekani imesema kuwa kwa kuwa gereza hilo liko nje ya Marekani basi katiba ya nchi hiyo haiwahusu.

Wakati huo huo Polisi nchini Ujerumani wamewakamata watu 22 wakishukiwa kujihusisha na mtandao haramu wa kimataifa wa kusafirisha watu.

Katika msako uliyofanyika kote Ujerumani usiku kwa wakati mmoja, zaidi ya polisi 350 walivamia madangulo, nyumba binafsi na kuwakata watu kadhaa kutoka Ujerumani, Poland na Bulgaria.

Wanatuhumiwa kwa kuwaingiza nchini Ujerumani wanawake wakiwemo wasichana wenye umri mdogo kufanyakazi za ukahaba