Wasiwasi juu ya Mjerumani na Wakorea walitekwa nyara nchini Afghanistan wazidi | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wasiwasi juu ya Mjerumani na Wakorea walitekwa nyara nchini Afghanistan wazidi

Baada ya kuuawa mteka mmoja wa Korea Kusini nchini Afghanistan, Korea Kusini imeongeza juhudi zake ili wengine Wakorea 22 ambao bado wako mikononi mwa watekaji nyara waachiliwe. Wakati huo huo, mazungumzo yanaendelea pia juu ya utekaji nyara wa Mjerumani mmoja mhandisi.

Wakorea wanadai jeshi lao liondoshwe kutoka Afghanistan

Wakorea wanadai jeshi lao liondoshwe kutoka Afghanistan

Licha ya muda wa mwisho uliotolewa kabla ya kuwaua mateka wengine 22 wa Korea Kusini kupita, Wataliban kwa mujibu wa msemaji wao, hawajamuua mwininge. Haya alisema msemaji wa Taliban Kari Mohammed Yussuf akizungumza na shirika la habari la Reuters. Jana, maiti ya kiongozi wa kundi hilo la Korea Kusini la kanisa la Presbyterian waliotoa misaada kwa wananchi imepatikana imetupwa jangwani ikiwa na majeraha ya risasi.

Korea Kusini leo wamemtuma Afghanistan mshauri wake wa taifa wa masuala ya usalama. Aidha, jamaa wa mateka hao wana wito kwa Wataliban kuwaachilia huru wafungwa wao. Katika barua yao, familia hizo walikumbusha kuwa mateka hao walitumia wakati wao nchini Afghanistan kuwasaidia wagonjwa. Kati ya mateka 22 waliosalia, 18 ni wanawake.

Wataliban walitaka wenzao wanaozuiliwa jela wanane waachiwe huru nchini Afghanistan. Serikali ya Kabul imepuuza dai hilo. Katika kesi nyingine ya utekaji nyara ya mwandishi wa habari kutoka Italy, serikali hiyo imewaachilia Wataliban watano na kukosolewa vikali kutoka nje.

Juu ya kutekwa nyara mhandisi wa Ujerumani, hakuna habari mpya hadi sasa. Wizara ya nje ya Ujerumani inafanya bidii kubwa, kama alivyothibitisha msemaji wa wizara hiyo, Gernot Jäger.

Kwa niaba ya serikali ya Ujerumani, Bw. Jäger aliwalaumu Wataliban kuendesha vita vya propaganda. Juu ya kufanya mashambulizi na kuwaua watu wasio na hatia, Wataliban pia wanatumia maneno kuendesha vita, alisema msemaji huyu Gernot Jäger: “Kuna mtu mmoja mwenye simu ya mkononi aliyeko katika eneo la mpaka kati ya Afghanistan na Pakistan na kwa kupiga simu mara moja tu anaweza kuiongofya nchi nzima ya Ujerumani. Hii haiwezekani, lakini serikali yetu itakataa kutimiza madai yao na kutishwa. Nchi za Kidemokrasi zinaweza kujeruhiwa, lakini zinaweza pia kujikinga.”

Bw. Jäger aliongeza kusema kuwa lengo la Wataliban ni kuwatisha watu na kuchochea hofu. Inabidi kutumia kila mbinu zilizopo kuzuia propaganda hiyo kufanya kazi.

Tena Wataliban si mafundi wasiojua kazi yao, ameonya Bw. Jäger: “Tunaweza kusema kuwa hao ndiyo bingwa wa mambo ya ugaidi. Wanaorodhesha maovu yao kwenye mtandao wa Internet, na vilevile wanaangalia kwa kina mijadala ya kisiasa inayoendelea barani Ulaya na kujaribu kuingilia kati. Mara nyingi tumeona kwamba taarifa zetu zimejibiwa haraka kutoka eneo hilo la mpakani mwa Afghanistan na Pakistan. Majibu haya yaonyesha kuwa watu hao wana habari kamili juu ya siasa na ripoti kwenye vyombo vya habari.”

Wakati huo huo mapigano dhidi ya wanangambo wa Wataliban yameendelea Kusini mwa Afghanistan. Kulingana na jeshi la Marekani, Wataliban wasiopungua 50 wameuawa katika muda wa saa 12. Kwa upande wa jeshi la kimataifa, mwanajeshi mmoja wa Uingereza ameuawa katika mapigano mahala pengine.

 • Tarehe 26.07.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHAS
 • Tarehe 26.07.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHAS

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com