1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON:Iraq na majirani zake kujadilia mustakabal wake

22 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBNa

Nchi ya Iraq na mataifa jirani wanakutana na viongozi wa ulimwengu kujadilia namna ya kuongeza kasi juhudi za kurejesha nchi hiyo katika hali ya kawaida.Visa vya ghasia zilizo na misingi ya kidini vinaendelea kutokea huku usalama ukiwa duni.Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon na Waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki wanaongoza kikao hicho cha mawaziri kinacholenga kuimarisha vikosi vya Umoja wa mataifa nchini humo aidha kujadilia mpango wa miaka 5 wa kustawisha nchi katika nyanja za uchumi,siasa na usalama.

Mkutano huo unafanyika baada ya Rais Goerge Bush wa Marekani kuonya kuwa vikosi vya marekani vitaendelea kubakia Iraq hata baada ya muhula wake kukamilika ifikapo mwaka 2009.Hata hivyo endapo hali ya usalama inaimarika majeshi alfu 169 yalioko huko huenda yakapunguzwa.

Majeshi yanayoongozwa na Marekani yalivamia Iraq mwaka 2003 mwezi wa machi ili kuondoa utawala wa marehemu Saddam Hussein.Kikao hicho kinahudhuriwa na wawakilishi kutoka mataifa 20 yakiwemo wanachama wa kudumu wa Umoja wa mataifa Uingereza,Uchina,Ufaransa,Urusi na Marekani vilevile nchi 8 jirani za Bahrain,Misri,Iran,Jordan,Kuwait,Saudia ,Syria na Uturuki.

Mkutano huo aidha unahudhuriwa na wawakilishi wa Canada,Ujerumani,Italia na Japan pamoja na Umoja wa Ulaya,Kamisheni ya Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Milki za Kiarabu .