1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washington.bush akutana na mjumbe maalum wa Sudan.

31 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CCxV

Rais wa Marekani George W. Bush hii leo anategemewa kukutana na mjumbe maalum wa Sudan, Andrew Natsios ili kupata taarifa mpya za maendeleo ya jitihada za kumaliza maafa katika jimbo la Darfur.

Rais Bush na mjumbe maalum Natsios watakutana katika ofisi za Ikulu ya Marekani mchana huu kuzungumzia migogoro ya kiutu katika jimbo lililoharibika kwa vita la Darfur, mazungumzo ambayo pia yatakuwa na lengo la kuhamasisha kupelekwa wanajeshi wa kulinda amani wa kimataifa.

Mkutano huu unakuja takriban wiki moja baada ya mshauri wa ulinzi wa serikali ya Marekani Stephen Hadley, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice, Andrew Natsios na naibu waziri wa mambo ya kigeni anaeshughulikia masuala ya Afrika Jendayi Frazer kuwa na mazungumzo Ikulu juu ya Darfur.

Natsios amerejea hivi karibuni akitokea Misri baada ya ziara yake ya wiki moja ya huko Sudan.

Hii ni ziara yake ya kwanza kikazi tangu pale Rais Bush alipomteuwa kuwa mjumbe maalum kuhusu Jimbo la Darfur mwezi September.