Wanigeria wapiga kura kuchagua rais wao
16 Aprili 2011Rais Goodluck Jonathan wa chama tawala cha People's Democratic (PDP) anachuana vikali na Meja Jenerali Mstaafu Muhammadu Buhari wa Congress for Progressive Change (CPC), Nuhu Ribadu wa Action Congress of Nigeria (ACN) na Ibrahim Shekarau wa All Nigeria People's Party (ANPP).
Buhari na Ribadu wanaonekana kutoa upinzani mkali kwa Rais Jonathan, lakini huenda rais huyo akashinda kwa kiwango kidogo. Buhari aliwahi kuwa rais aliyeingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi hapo mwaka 1983 kabla naye kupinduliwa na Jenerali Ibrahim Babangida miaka miwili baadaye.
Ribadu ndiye mgombea kijana kabisa akiwa amezaliwa mwaka 1960, na ndiye aliyekuwa mkuu wa kamisheni ya kupambana na ufisadi nchini Nigeria, ambayo ilichukua hatua kali dhidi ya mafisadi nchini humo baina ya mwaka 2005 na 2006.
Uchaguzi wa leo unatarajiwa kurejea mafanikio ya uchaguzi wa bunge wa wiki iliyopita, ambao pamoja na matukio ya hapa na pale, umetajwa kuwa ulikuwa mzuri zaidi kulinganisha na chaguzi zilizopita kwenye nchi hiyo.