1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wananchi waupokea utawala wa kijeshi, Niger

21 Februari 2010

Siku mbili baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Niger utawala huo wa kijeshi umeahidi kuandaa uchaguzi.

https://p.dw.com/p/M70m
Wananchi wa Niger waunga mkono mapinduzi.Picha: AP

Utawala mpya wa Kijeshi nchini Niger umeahidi kuwa nchi hiyo itaandaa uchaguzi, lakini hawakutaja tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo. Tangazo hili lilitolewa wakati viongozi hao wa Kijeshi walipojitokeza hadharani, huku wananchi wa Niger wakiandamana kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Mamadou Tandja siku mbili zilizopita.  Kulingana na Kanali Djribrilla Hamidou Hima mmoja wa viongozi hao wa kijeshi, utawala huo mpya kwanza unataka kusuluhisha mzozo wa kisiasa nchini humo kabla ya kuandaa uchaguzi. Upinzani nchini Niger pamoja na Jumuiya ya Kimataifa wameushinikiza utawala huo wa kijeshi uliomuondoa madarakani Rais Tandja kupanga uchaguzi ili kuirejesha Niger katika utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo. Mapinduzi hayo ya kijeshi yamelaaniwa na Jumuiya ya Kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Niger / Tandja / Putsch
Rais aliyepinduliwa Mamadou Tandja.Picha: AP