1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Ujerumani wawasili Lithuania

Mohammed Khelef
9 Aprili 2024

Viongozi wa Lithuania wamepongeza kile walichokiita "tukio la kihistoria" baada ya Ujerumani kutuma wanajeshi wake kwenye taifa hilo la Baltiki lililo mwanachama wa Muungano wa Kijeshi wa NATO.

https://p.dw.com/p/4eYxa
Boris Pistorius Ujerumani
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius (katikati), akiwaaga wanajeshi wa nchi yake waliopelekwa Lithuania.Picha: Lisi Niesner/REUTERS

Hii ni mara ya kwanza tangu Vita vya Pili vya Dunia kwa wanajeshi wa Ujerumani kutumwa nje ya nchi kwa ajili ya kukaa muda mrefu.

Wanajeshi wapatao 24 waliwasili nchini Lithuania siku ya Jumatatu (Aprili 8), wakiwatangulia wenzao 150 ambao watajiunga nao baadaye mwaka huu.

Soma zaidi:Wanajeshi wa Ujerumani wawasili Lithuania, kwa mara ya kwanza tangu Vita vya Pili vya Dunia 

Idadi kamili ya wanajeshi wa Ujerumani watakaopelekwa nchini humo itakuwa 5,000 kufikia mwishoni mwa mwaka 2027.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, aliwaaga wanajeshi hao mjini Berlin, akisema ilikuwa ni "siku muhimu" kwa jeshi la nchi yake, Bundeswehr.

Mjini Vilnius, Waziri wa Ulinzi Laurynas Kasciunas, aliwapokea wanajeshi  hao akisema ni mfano mzuri kwa mataifa yote wanachama wa NATO upande wa mashariki mwa Ulaya, yanayopakana na Urusi na mshirika wake, Belarus.