1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walinda amani wa DRC na tuhuma za ubakaji

Sylvia Mwehozi
8 Juni 2017

Kamanda wa kikosi hicho anasema mamia ya wanajeshi hao wanaotuhumiwa kwa vitendo vya ubakaji huenda wakarejeshwa nyumbani ikiwa nidhamu yao haitaimarika. 

https://p.dw.com/p/2eLT9
Zentralafrikanische Republik UN Soldaten
Picha: picture-alliance/AA/H. Serifio

Umoja wa Mataifa umesema nyaraka zilizovuja zikikosoa tabia za wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walioko katika kikosi cha kulinda amani katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, ilikuwa ni sehemu tu ya tathmini ya kawaida. 

Nyaraka za tathmini hiyo ndefu yenye kurasa 68 na inayotoa wito wa kurejeshwa nyumbani kwa wanajeshi wa Congo katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiwa hawataboresha "viwango" vya kikosi hicho, kwa mara ya kwanza ilivuja siku ya Jumanne.

Luteni Jenerali Balla Keita, kamanda wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani katika taifa hilo aliandika kwamba wanajeshi wa kutoka Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo "hawaaminiki tena kutoka na uongozi mbovu, ukosefu wa nidhamu na kutowajibika ipasavyo".

Zentralafrikanische Republik UN-Kräfte Minusca
Kikosi cha MINUSCA Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Pia alibainisha kwamba kikosi hicho kimekuwa na "sifa mbaya" ya unyanyasaji wa kingono pamoja na uuzaji wa mafuta katika taarifa ya tarehe 12 Mei ambayo ilichapishwa na kampeni ya Code Blue inayoongozwa na shirika lisilo la kiserikali linalopigania uwajibikaji wa walinda amani. Keita anaripotiwa kuwa tayari amependekeza kikosi kizima kurejeshwa nyumbani.

"Congo inapaswa kuwajibika katika kujiboresha bila ya kuchelewa nidhamu ya kiksoi chake. Ikiwa sivyo, kwanza uamuzi utafanyika wa kuwarejesha nyumbani na kubadilisha kikosi cha Congo, ilisema taarifa ya kamanda huyo. Kamanda huyo tayari ametuma barua sita za madai kwa kamanda wa kikosi cha Congo ndani ya mwaka huu pekee.

Kikosi hicho chenye kituo chake katika mji wa Berberati huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, pia kinakabiliwa na tuhuma za usafirishaji wa mafuta na kamanda Keita alibainisha hilo katika taarifa ya mwezi Mei na kwamba ni magari machache kati ya 114 yanoyofaa. 

Wanajeshi 120 katika kikosi hicho walirudishwa nyumbani mwaka jana katika msingi wa madai ya ukosefu wa nidhamu, kwa mujibu wa tathmini hiyo.

Hapo jana, msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema ripoti inaonyesha kwamba kamanda Keita alikuwa akitimiza wajibu wake na tathmini hiyo ni utaratibu wa kawaida. Idara ya Umoja wa Mataifa ya operesheni za kulinda amani pia ilisema katika taarifa yake kuwa imeipokea ripoti hiyo na imeisambaza  kwa wanachama na inafuatilia njia za kuchukua.

Zentralafrikanische Republik Blauhelmsoldat
Askari wa MINUSCA akimkagua raia kabla ya kuingia kituo cha kupigia kura CARPicha: Getty Images/AFP/M. Longari

Takwimu za Umoja wa Mataifa zimeonyesha kuwepo na matukio matatu yanayohusisha wanajeshi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya congo mwaka huu na tisa yaliripotiwa mwaka jana. Madai ya unyanyasaji wa kingono pia yalielekezwa kwa wanajeshi wa kulinda amani kutoka nchi za Burundi na Gabon katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mnamo mwezi Desemba.

Mapema mwaka huu, Gutterres alizindua mkakati mpya wa kukomesha unyanyasaji wa kingono unaofanywa na wale wanaotumika chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa una wanajeshi 13,000 huko Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao wanafanya kazi ya kurejesha amani baada ya taifa hilo kukumbwa na machafuko ya kidini.

mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters/DpA

Mhariri: Saumu Yusuf