Wakuu wa Ulaya wakutana tena kuijadili euro | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.10.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wakuu wa Ulaya wakutana tena kuijadili euro

Jumapili unafanyika mkutano wa mataifa yanayotumia sarafu ya euro kujadili mgogoro wa madeni katika eneo lao, lakini tayari wasiwasi umeanza kuzuka ikiwa patafikiwa makubaliano yoyote kuhusiana na dhima za mfuko wa EFSF.

Kansela Angela Merkel (kulia) na Rais Nicolas Sarkozy.

Kansela Angela Merkel (kulia) na Rais Nicolas Sarkozy.

Tayari imeshaamuliwa kuwa kutakuwa na mkutano mwengine hapo Jumatano mjini Brussels, kabla ya hata huu wa Jumapili kufanyika. Sababu ni kuwa pana uwezekano mdogo sana kwa muafaka kupatikana. Ufaransa na Ujerumani, ambayo ndiyo mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi kwenye eneo la euro, hazijakubaliana hadi sasa.

Mkuu wa mambo ya uchumi kwenye Umoja wa Ulaya, Olli Rehn, ameyataka mataifa hayo kukubaliana haraka iwezekanavyo, vyenginevyo mgogoro huu hauwezi kutatuliwa.

"Suala hili lazima liamuliwe kwa haraka na kwa uhakika. Hicho ndicho ambacho makampuni, benki na mabunge kinayatarajia, yaani kuwa na mfumo makini, mwepesi, ulio wazi na unaowajibika." Amesema Michel Barnier wa Soko la Ulaya.

Masoko ya hisa Ulaya yapanda

Bendera za baadhi ya mataifa ya Umoja wa Ulaya

Bendera za baadhi ya mataifa ya Umoja wa Ulaya

Lakini wakati kukiwa na wasiwasi huo, leo masoko ya hisa barani Ulaya yamepanda juu kidogo. Jijini London, hisa zilipanda kwa asilimia 0.36, mjini Frankfurt kwa asilimia 0.58 na Paris kwa asilimia 0.86.

Mkutano wa Jumapili unatarajiwa kuutathmini mfuko wa kuinusuru sarafu ya euro, lakini baadhi ya wachambuzi wanaouna ni kupitisha muda tu kabla ya ule wa mataifa 17 ya euro, utaofanyika Jumatano. Hii inawezekana ikawa ndiyo sababu ya mkutano wa kibiashara kati ya Ulaya na China uliokuwa ufanyike Jumanne nchini Chini kuahirishwa.

Mkutano huo pia unatakiwa uje na mpango mzima wa kulitatua tatizo la madeni kwenye Umoja wa Ulaya, na kueleza namna ambavyo Ugiriki itaweza kujinasua kwenye dimbwi la madeni hatua kwa hatua. Mkutano huu pia unatakiwa kuja na mipango ya kuzifanya benki za Ulaya kuwa na uwezo wa kuhimili mtikisiko wa kiuchumi.

Ujerumani na Ufaransa hazijakubaliana

Kansela Angela Merkel (kushoto) na Rais Nicolas Sarkozy.

Kansela Angela Merkel (kushoto) na Rais Nicolas Sarkozy.

Kikwazo, hata hivyo, kimekuwa na kinaendelea kubakia kuwa Ujerumani na Ufaransa, ambapo kila mmoja amekuwa na mtazamo wake kuhusiana na dhima ya mfuko wa kuikoa sarafu ya euro, EFSF. Wakati Ufaransa inataka mfuko huo uelekezwe kwenye benki ambazo zitakuwa na uwezo wa kukopa zitakavyo kutoka Benki Kuu ya Ulaya, Ujerumani haikubaliani kabisa na wazo hilo.

"Ufaransa na Ujerumani zimepiga hatua kubwa kufikia makubaliano, lakini hazitoshi kufikia maamuzi. Ndio maana tutakuwa na mazungumzo Jumapili hii, lakini tutafanya maamuzi Jumatano". Amesema msemaji wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Steffen Seibert.

Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya yanataka benki na sekta binafsi kushiriki moja kwa moja kwenye mgogoro wa madeni ya Ulaya, ikiwemo kukubali kupoteza kwenye deni la Ugiriki, kabla ya mabilioni ya euro kukubaliwa kuiokoa nchi husika.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA
Mhariri: Saumu Yusuf

DW inapendekeza

 • Tarehe 21.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12wO4
 • Tarehe 21.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12wO4

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com