1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mmkutano wa G20 kujadili mzozo wa kanda ya euro

14 Oktoba 2011

Mawaziri wa fedha na viongozi wa benki kuu wa kundi la nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda na zinazoimarika kiuchumi duniani-G20 wanakutana leo hii katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris.

https://p.dw.com/p/Rqqu
Finance ministers and central bank governors pose for a group photo during the G20 Finance summit at Bercy Finance Ministry in Paris, France, Saturday, Feb. 19, 2011. Finance chiefs from the world's 20 most industrialized and fastest developing nations wrestle over how to steady the world economy at a two-days meeting in Paris. (AP Photo/Francois Mori)
Mawaziri wa Fedha na viongozi wa Benki Kuu wa kundi la G20Picha: AP

Lengo kuu la mkutano huo ni kuandaa mkutano wa viongozi wa taifa na serikali wa kundi hilo la G20 utakaofanywa mwezi wa Novemba mjini Cannes. Lakini, mkutano wa leo utashughulikia pia mzozo wa kanda ya euro unaohusika na Ugiriki na madeni ya nchi zingine za kanda ya euro. Mzozo wa kanda ya euro unazidi kuathiri ukuaji wa kiuchumi duniani, kwa hivyo ni matumaini ya mawaziri wa nchi zilizo nje ya Ulaya katika kundi hilo la G20, kuwa washirika wenzao barani Ulaya watathibitisha kuwa kila kiwezekanacho kinafanywa kuudhibiti mzozo huo. Wasiwasi ukizidi kuathiri maeneo mengine duniani, mawaziri wanaotoka nje ya Ulaya wanatazamiwa kuzungumza waziwazi kuhusu mzozo wa kanda ya euro.

Waziri wa Fedha wa Canada Jim Flaherty tayari alifanya hivyo hapo jana kabla ya kuondoka Ottawa kuelekea Paris. Yeye alisema, mzozo huo haushughulikiwi vya kutosha na kanda ya euro. Kuna hatari ya mtengano kutokea katika mkutano wa leo huku nchi za Ulaya zikikosolewa na mataifa mengine kuwa zinashindwa kuudhibiti mzozo wa madeni ulioanza tangu miezi kumi na nane iliyopita. Hiyo ni kinyume kabisa na mwaka 2009, ambapo nchi za G20 zilishirikiana kuanzisha mradi uliolenga kuufufua uchumi duniani.

FILE - Olli Rehn, the European Commissioner for Economic and Financial Affairs gives the EU Spring forecast 2011-12 during a news conference at the EU council headquarters in Brussels, Belgium, 13 May 2011. European Union Economy Commissioner Olli Rehn criticized Greece on Monday, May 16, 2011 for its slow pace of reform, only hours before eurozone finance ministers were due to discuss the country's debt problems at a meeting in Brussels. EPA/OLIVIER HOSLET +++(c) dpa - Bildfunk+++
Mkuu wa masuala ya uchumi na fedha wa Umoja wa Ulaya, Olli RehnPicha: picture alliance/dpa

Ujerumani na Ufaransa zinachukua muda kukubaliana njia ya kuongeza mitaji ya benki. Vile vile nchi hizo mbili zenye uchumi mkubwa katika kanda ya euro, zinatofautiana katika suala la kudhamini hati za pamoja katika kanda ya euro, kwani Ujerumani haitaki kuongeza mzigo wa madeni yake. Hata hivyo kiini cha mpango wo wote ule, ni makubaliano kuhusu njia ya kuuimarisha mfuko wa msaada wa dharura EFSF, kwa nchi zilizokumbwa na madeni. Kwa maoni ya mkuu wa masuala ya uchumi na fedha wa Umoja wa Ulaya, Olli Rehn,sekta ya binafsi pia inapaswa kusaidia. Amesema:

"Ni muhimu kwa sekta ya binafsi pia kubeba sehemu ya mzigo huo, kama serikali na wanalipa kodi wanavyofanya kwa kudhamini mikopo kwa ajili ya Ugiriki."

Wataalamu wa Ujerumani na Ufaransa wapo mbioni kutayarisha mswada wa dharura kabla ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya hapo Oktoba 23. Mzozo wa kanda ya euro umesababisha thamani ya hisa kuporomoka katika masoko ya fedha. Wawekezaji pia hawana tena imani na masoko ya fedha kwa sababu ya wasiwasi juu ya uwezekano wa Ugiriki na hata nchi zingine kufilisika.

Njia ya kupambana na ukosefu wa usawa katika uchumi wa dunia, jitahada za kufanya mageuzi katika mfumo wa sarafu duniani na kuanzisha sheria za kudhibiti biashara za fedha zinazopindukia viwango pamoja na taasisi za fedha, ni mada zilizo katika ajenda ya mkutano wa mawaziri wa fedha wa G20 unaoanza leo jioni mjini Paris.

Mwandishi: Martin,Prema rtrd/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef