Wahariri watoa maoni yao juu ya mjadala ufa uliojitokeza miongoni mwa nchi zinazopambana na Gaddafi | Magazetini | DW | 22.03.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Wahariri watoa maoni yao juu ya mjadala ufa uliojitokeza miongoni mwa nchi zinazopambana na Gaddafi

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni juu ya mgawanyiko katika mfungamano wa nchi zinazomkabili Kanali Gaddafi

Ndege za kijeshi za mataifa ya magharibi zikielekea Libya

Ndege za kijeshi za mataifa ya magharibi zikielekea Libya

Wakati ndege za nchi za magharibi zinaendelea kumshambulia Gaddafi, umetokea mjadala miongoni mwa nchi hizo juu ya nani anapaswa kuongoza kampeni dhidi ya kiongozi huyo wa Libya.

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni yao.

Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya mchango wa Ujerumani kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Juu ya kile kinachoweza kuitwa ufa katika ukuta wa nchi za magharibi zinazomkabili Gaddafi, gazeti la Badische linasema, hakika kila mtu angelipendelea kujua ni nani hasa anaiongoza kampeni dhidi ya Gaddafi.

Marekani imesema haitaki, jumuiya ya Nato imegawanyika, na wazo la Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy kwamba Umoja wa Ulaya unaweza kulichukua jukumu la kuongoza harakati dhidi ya Gaddafi, linapaswa kuchukuliwa kama mzaha.

Mhariri wa gazeti la Badische anasema ikiwa wote wamekataa,waliobakia ni Uingereza na Ufaransa. Lakini panapohusu kutafakari sera na mikakati, Rais wa Ufaransa mpaka sasa bado hajaonyesha umaarufu.

Naye mhariri wa gazeti la Westdeutsche anakumbusha kwamba wakati madola ya Nato yanabishana juu ya uongozi , vijana wao wanahatarisha maisha yao !

Gazeti hilo linaeleza kuwa Gaddafi amegeuka kuwa mtihani kwa nchi za NATO.

Kila siku inayopita kwa kuzozana juu ya suala la uongozi Nato inapoteza imani duniani.

Lakini mhariri anasema , jambo moja asilani lisisahauliwe kwamba wanajeshi kutoka nchi kadhaa za Nato wanayahatarisha maisha yao katika juhudi za kulitekeleza azimio la Baraza la Usalama.

Gazeti la Südwest Presse linalalamika juu ya siasa ya mambo ya nje ya serikali ya mseto ya Ujerumani inayoongozwa na Kansela Angela Merkel.Gazeti hilo linasema ilikuwa hatua ya mafanikio kwa Ujerumani kupata kiti kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Lakini haukupita hata mwezi mmoja , Ujerumani ilianza kushika njia yake peke yake.

Na kauli zote zinazotolewa na Kansela pamoja na waziri wake wa mambo ya nje haziwezi kuuficha ukweli kwamba msimamo wa Ujerumani duniani, ni mgumu kueleweka kwa wajerumani na kwa washirika wake wa kimataifa.


Mhariri wa gazeti la Märkische Oderzeitung anatoa maoni juu ya hali ya nchini Yemen.

Anasema utawala wa rais Ali Saleh unakaribia mwisho. Siyo tu kwa sababu watu mashuhuri nchini Marekani wanajitenga na rais huyo, bali pia kwa sababu majenerali wake wanampa kisogo.

Gazeti la Badische Neueste Nachrichten linauzungumzia mgogoro wa Libya.

Linatilia maanani kwamba watu wa mji wa Beghazi wameupokea msaada wa Ufaransa kwa moyo mkunjufu, kiasi kwamba wanaipeperusha bendera ya Ufaransa.

Mwandishi/Mtullya Abdu /Duetsche Zeitungen/

Mhariri/Yusuf Saumu Ramadhani

 • Tarehe 22.03.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/10fPa
 • Tarehe 22.03.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/10fPa