1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Wahariri watoa maoni juu ya Merkel na Sarkozy

Wahariri wanazungumzia mkutano wa kwanza mwaka huu wa viongozi wa mataifa mawili yenye nguvu katika Umoja wa Ulaya, Kansela Merkel wa Ujerumani na Rais Sarkozy wa Ufaransa, kuujadili mgogoro wa madeni wa Umoja huo.

French President Nicolas Sarkozy (L) and German Chancellor Angela Merkel smile as they address a news conference following their talks at the Chancellery in Berlin January 9, 2012. REUTERS/Fabrizio Bensch (GERMANY - Tags: POLITICS)

Kansela Merkel na Rais Sarkozy

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanauzingatia umuhimu wa mkutano huo uliofanyika mjini Berlin.

Mhariri wa Märkische Allgemeine anaesema kuwa ni jambo zuri kwamba Ujerumani na Ufaransa, yaani majirani, wanakubaliana juu ya masuala muhimu yanayohusu kuiokoa sarafu ya Euro.

Mhariri wa Märkische Alllgemeine anatilia maanani kwamba Sarkozy na Merkel wanakubaliana pia juu ya kuanzishwa kodi ya shughuli za kifedha. Sarkozy anataka kodi hiyo ianzishwe haraka.

Gazeti la Volksstimme linasema katika maoni yake kwamba Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, aliitumia fursa ya mkutano wa jana kumuunga mkono Rais wa Ufaransa katika juhudi zake za kutaka kodi ya shughuli za kifedha ianzishwe mara moja.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa mwezi wa Desemba mwaka jana, Rais Sarkozy aliiunga mkono sera ya Ujerumani ya ubanaji wa matumizi.

Gazeti linasema jana ilikuwa zamu ya Kansela wa Ujerumani, bibi Merkel, kujitokeza wazi na kumuunga mkono Rais Sarkozy juu ya suala la kodi ya shughuli za kifedha. Mhariri wa Volksstimme anasema kodi hiyo ni muhimu sana kwa sababu, kwa kodi hiyo, mabenki pia yatashiriki katika juhudi za kuziokoa nchi zenye madeni katika Umoja wa sarafu ya Euro.

Gazeti la Mitteldeutsche linauzingatia mkutano baina ya Kansela wa Ujerumani na Rais wa Ufaransa katika muktadha wa uchaguzi wa Rais nchini Ufaransa. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba Merkel anamuunga mkono Rais Sarkozy anaetaka kuonyesha mafanikio katika juhudi za kupambana na mgogoro wa madeni barani Ulaya. Merkel anajua kwa nini anafanya hivyo.

Gazeti la Mitteldeutsche linatilia maanani kwamba haitakuwa rahisi kwake ikiwa mgombea urais wa chama cha wasoshalisti- Hollande- atashinda.Jukumu la kuukabili mgogoro wa madeni litakuwa gumu baina ya Ujerumani na Ufaransa ikiwa msoshalisti huyo atakuwa Rais.

Mhariri wa gazeti la Hessische/Niedersächsische anasema mkutano wa jana umethibitisha jinsi Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na Rais wa Ufaransa wanavyotegemeana. Kwani bila ya kusimama kwenye jukwaa la pamoja, Umoja wa sarafu ya Euro utabakia katika kurasa za vitabu vya historia.

Gazeti hilo linasema Kansela wa Ujerumani hana njia nyingine. Anajua kwamba ikiwa Ujerumani na Ufaransa hazitasimama pamoja juu ya masuala muhimu ya Ulaya ,basi mradi unaoitwa sarafu ya Euro utatoweka, lakini pia Rais Sarkozy atasahauliwa ikiwa hatafanikiwa kuunadi kwa watu wake mpango wake wa kuanzisha kodi ya shughuli za kifedha. Mkutano wa jana ulikuwa wa manufaa kwa pande zote mbili.

Mwandishi:Mtullya, Abdu
Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 10.01.2012
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/13hBk
 • Tarehe 10.01.2012
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/13hBk