1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyabiashara waingiza bidhaa za chakula Zimbabwe.

Mohamed Dahman16 Agosti 2007

Masoko ya mitumba yanayonawiri katika mji wa Bulawayo ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Zimbabwe yamekuwa vituo vya biashara na fedha ambapo wafanyabishara wanaovuka mipaka huuza bidhaa zao na pia kuwa chimbuko la fedha za kigeni.

https://p.dw.com/p/CHji
Wakaazi wa Harare wakiwahi madukani kununuwa bidhaa kufuatia agizo la serikali la kushusha bei kwa nusu lililopelekea mashubaka kuwa matupu madukani.
Wakaazi wa Harare wakiwahi madukani kununuwa bidhaa kufuatia agizo la serikali la kushusha bei kwa nusu lililopelekea mashubaka kuwa matupu madukani.Picha: AP

Kwa wakaazi wengi wanaotapia maisha katika mazingira magumu ya kiuchumi huku kukiwa na uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu wafanyabishara wa kuvuka mipaka wamekuwa wasambazaji pekee wa chakula nchini humo.

Mbali na bidhaa za vyakula na bidhaa nyengine ndogo ndogo nguo za bei rahisi kutoka Bhotswana ambazo zimeagiziwa kutoka China ni bidhaa nyengine muhimu inayouzwa kwenye masoko ya mitumba ya mji wa Bulawayo.

Sithabile Khuzwao ni mmojawapo ya wanawake wengi ambao huingiza kwenye mji huo bidhaa hizo za vyakula na bidhaa nyengine ndogo ndogo pamoja na nguo kutoka nchi jirani za Bhotswana na Afrika Kusini.

Hata hivyo ameliambia shirika la habari la IPS kwamba uhasama kati ya wananchi wa Bhotswana na wafanyabishara wa Zimbabwe umefanya ununuzi wa bidhaa nchini Bhotswana kuwa ni jambo la hatari.Anasema kabla ya kuanza kwa matatizo ya Zimbabwe walikuwa wakiweza kuzunguka nchini humo bila ya matatizo lakini sasa wamekuwa wakiandamwa na baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakivamiwa na kuibiwa bidhaa zao na Wabatswana.

Mazingira magumu ya kiuchumi yamepelekea wanawake wengi kutumbukia kwenye sekta ya biashara isio rasmi katika mji wa Bulawayo mji wenye wakaazi zaidi ya milioni mbili.Hivi karibuni hata watu wenye uzoefu wa kazi kama vile walimu na waauguzi wamejiunga katika mkumbo huo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

Katika kituo cha mpakani cha Plumtree ambapo maelfu ya Wazimbabwe wanavuka mpaka kuingia Bhotswana kila wiki wafanyabiashara wanasema hali ya kuhamisha bidhaa inazidi kuwa ngumu.Bidhaa za vyakula hivi sasa zimekuwa haba nchini Zimbabwe baada ya agizo la serikali kuwalazimisha wenye maduka ya reja reja kupunguza bei kwa nusu.Hatua hiyo imesababisha mashubaka ya maduka kuwa matupu.

Kulizuka hofu mwezi uliopita wakati serikali ya chama cha ZANU-PF ilipotangaza upigaji marufuku uingizaji wa bidhaa za chakula kutoka nchi jirani ikiwa ni sehemu ya hatua yake ya kupunguza bei za bidhaa.Bila ya kutowa ufafanuzi serikali iliwashutumu wafanyabiashara kwa kuchochea uhaba wa bidhaa muhimu.

Serikali ilitenguwa agizo hilo baada ya wananchi kulalamika. Uuzaji wa bidhaa katika mitaa ya Bulawayo kama vile mafuta ya kupikia,unga wa mahindi, viatu na nguo kutoka Botswana unaonyesha kwamba biashara isio rasmi ya kuvuka mipaka inaendelea licha ya matatizo yanayowakabili maelfu ya wanawake ambao wamegunduwa njia ya kujinusuru kwenye maisha katika sekta hii.

Wafanyabishara hao wanataja ushuru mkubwa unaotozwa na forodha ya Zimbabwe kuwa mojawapo ya sababu ya kuingiza bidhaa chache nchini mwao.

Portia Zuse mwenye umri wa miaka 27 ameliambia shirika la habari la IPS kwamba ametakiwa kutowa fedha katika forodha ambazo thamani yake ilikuwa sawa na bidhaa alizonunuwa nchini Botswana jambo ambalo amesema kibiashara linakuwa halina maana kabisa kwani inabidi ajipatie chochote kwa safari zake hizo.

Zimbabwe na Botswana zimesaini makubaliano ya nchi mbili juu ya kuepuka utazaji kodi maradufu kama sehemu ya kile Zimbabwe inachoona kuwa ni hatua ya kuimarisha biashara kupitia mipaka.

Hata hivyo habari hizo zinaonyesha kwamba serikali ya Zimbabwe bado ingali inayafanya maisha ya wafanya biashara ndogo ndogo wa kuvuka mipaka kuwa magumu.