1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Libya waendelea kupambana dhidi ya vikosi vya Gaddafi

Saumu Ramadhani Yusuf28 Aprili 2011

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC inayoshughulikia uhalifu,Moreno Ocampo anajiandaa kuwasilisha ripoti yake ya uchunguzi mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Libya.

https://p.dw.com/p/115YB
Waasi wa LibyaPicha: picture alliance / dpa
Taarifa za hivi punde zinasema kwamba Mapigano makali yamezuka kati ya waasi na vikosi vya kanali Gaddafi kwenye eneo la mpaka wa Libya na Tunisia katika mji wa Dehiba uliokuwa umetwaliwa na waasi hapo jana.Wakati huohuo imearifiwa kwamba mjumbe wa Libya katika Umoja wa Mataifa Abdul Illah al Khatib amefanya mazungumzo hii nchini Uturuki na kujadili kuhusu hali inavyotisha nchini Libya kabla ya kwenda Benghazi.

Moreno Ocampo anaendelea na uchunguzi wake juu ya uhalifu wa ubinadamu unaodaiwa kuendelea nchini Libya kufuatia mapambano yanayoshuhudiwa kati ya vikosi vya Kanali Muammar  Gaddafi na waasi wanaosaidiwa na vikosi vya jumuiya ya kujihami ya NATO.Uchunguzi huo wa Ocampo mbali na Kanali Gaddafi na wanawe watatu unawalenga pia maafisa wanne wa Libya akiwemo mwanadiplomasia wa ngazi ya ju Mussa Kussa na aliyekuwa waziri mkuu Abu Zayd Omar Dorda,mkurugenzi mkuu wa shirika la usalama wa ndani nchini Libya.Kwa hivi sasa ndani ya Libya kwenyewe waasi wanaendelea kupambana kuukomboa uwanja wa ndege wa Misrata baada ya kuwasogeza nyuma wanajeshi wa Kanali Gaddafi kutoka kwenye bandari ya mji huo huku viongozi wa kikabila nchini humo wakimtaka Gaddafi aondoke madarakani.Kumesikika mripuko mkubwa mjini Tripoli mara tu baada ya ndege za NATO kuruka kwenye anga ya mji huo mkuu wakati waasi nao wakiomba msaada zaidi wa silaha nzito nzito kutoka nchi za Magharibi wamesema ''Nato imefanya vizuri lakini tunahitaji msaada zaidi kuwamaliza wanajeshi wa Kanali Gaddafi''

Waasi katika eneo hilo la Misrata wamesema wanaimani kwamba wanakaribia kuupata ushindi  katika mji huo wa Misrata.Wakati hayo yakiendelea maelfu ya wakimbizi wanaendelea kuyakimbia maeeneo hatari huko Magharibi ya Libya huku wakitoa mwito wa vita kumalizwa haraka kutokana na madhila wanayoyapata zaidi kina mama na watoto katika eneo hilo.

Ama upande mwingine mjini Brussels kumefunguliwa taasisi inayowaunga mkono waasi ikiwa na lengo la kufanikisha mawasiliano kati ya Umoja wa Ulaya na jumuiya ya Nato na waasi wa Libya katika harakati za kuelekea kuikomboa Libya na kuleta demokrasia.

Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE

Mhariri Josephat Charo.