1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za rimoti katika uandishi habari

Yusra Buwayhid
30 Aprili 2018

Ndege zinazoendeshwa kwa rimoti na satalaiti zinalisaidia bara la Afrika kufichua mambo yasio ripotiwa katika vyombo vya habari hasa katika maeneo yaliyo vigumu kufikiwa. Hata hivyo sheria dhidi yake zimeshaanza kuwekwa.

https://p.dw.com/p/2ww2c
Afrika Drohnen
Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Farrell

Kwa mwanahabari wa mjini Nairobi, Soila Kenya teknolojia ni njia ya kufichua ukweli. Akikumbuka shambulio la kundi la kigaidi la al-Shabab la 2017, wakati wanamgambo walipovamia kambi ya kijesjhi ya Kulbiyow, Somalia, wakati vikosi vya usalama vya Kenya vilipoficha ukweli wa athari za shambulio hilo na kusema kwamba walifanikiwa kuwafukuza washambuliaji. Lakini picha zilizonaswa na ndege zinazorushwa kwa rimoti pamoja na teknolojia ya satalaiti zilionesha hali nyingine kabisa.

Wachambuzi kutoka Shirika la Uchunguzi wa Ulinzi wa Afrika pamoja na kundi la utafiti wa taarifa za mitandaoni la Bellingcat wamegundua kwamba wanamgambo hao walifanya uharibifu mkubwa katika kambi hiyo pamoja na kujeruhi watu.

"Teknolojia ya satalaiti ilifichua kitu ambacho venginevyo kisingejulikana," amesema mwanadishi habari Soila Kenya.

Kuthibitisha ukweli sio eneo pekee ambalo teknolojia inaweza kusaidia katika kazi ya kuripoti taarifa. Ndege zisizokuwa na rubani zinafika maeneo ambayo vigumu kufikiwa na binadamu kwa miguu," anasema mwandishi habari wa Afrika Kusini na mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Code for Afrika Justin Arenstein. Kwa mfano, vita vya wenyewe kwa wenyewe vya nchini Syria vimepata umaarufu zaidi kuliko vita vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, anasema.

Ingawa kuna harakati kubwa za watu nchini humo, na idadi kubwa ya ripoti za idadi ya vifo vya raia kutoka nchini Congo, lakini vita hivyo havipati kipaumbele kwa sababu hakuna ushahidi wa picha wa kuonesha hasa kinachotokea nchini humo, ameongeza.

WorldLink, drones, Uganda, Asaph Kasujja
Mtumiaji wa ndege za rimoti Kampala, UgandaPicha: Jeroen van Loon

Teknolojia inaweza kusaidia kuyasogeza mbele masuala ambayo hayaripotiwi vya kutosha. Mradi mmoja umefuatilia suala la upokonyaji wa ardhi katika Hifadhi ya Taifa ya Kruger Afrika Kusini. Picha za satalaiti na vidio zilizovutwa kwa kutumia ndege zisizo na rubani na zinazotumia rimoti, zimeonyesha jinsi watu wanavyofukuzwa katika jamii hiyo ili mabilionea wapate ardhi ya kuongeza maeneo ya hifadhi hiyo.

Mradi mwengine umetumia vipaza sauti vya chini ya maji kufichua uvuvi haramu unaofanywa katika pwani ya Tanzania na kuharibu makaazi ya viumbe wa baharini. Kifaa hicho kinapogundua mripuko chini ya maji, ndege isiyo na rubani inatumwa na timu ya maripota inatumiwa taarifa ya kufika katika eneo hilo.

Najaribu kutumia kifaa kipya cha teknolojia kufuatilia tatizo kongwe na la muda mrefu, anasema mpiga picha Johnny Miller, mwanzilishi wa shirika lisilo na faida la AfricanDrone, ambaye anatumia kamera zilizofungwa kwenye ndege zinazorushwa kwa rimoti kukusanya data za suala la ukosefu wa usawa Dar es Salaam Tanzania, na Nairobi, Kenya. Mradi huo pia umesambaa kutoka Mexico hadi Marekani, anasema.

Lakini taarifa hizo sio mpya. Afrika Kusini, ambako Miller alianzia kazi yake hiyo, imetajwa na benki ya Dunia mwaka 2017 kuwa nchi inayoongoza kwa kukosa usawa duniani kote. Picha za Miller zinaonyesha tofauti kati ya majumba makubwa ya kifahari yaliyojengwa pembezeno mwa makaazi ya mitaa ya ovyo. Picha zinazoonyesha mtazamo tofauti ambao nadra kuonekana.

Sababu moja iliyopelekea  ndege zinazotumia rimoti kuweza kutumika kwa haraka ni ukosefu wa sheria za kuzuia utumiaji wake. Lakini hilo linaelekea kubadilika. Afrika Kusini ilikuwa ni nchi ya kwanza miongoni mwa mataifa yaliyo Kusini mwa Jangwa la Sahara kuweka kanuni za kudhibiti haki za waruashaji wa ndege hizo, kwa kuwalazimisha kupitia mchakato mrefu na wenye gharama wa kujisajili na kupata cheti.

Nchi nyingine za Kiafrika zinaonekana kufwata mfano wa Afrika Kusini. Kenya na Tanzania, kwa mfano, zinawalazimisha marubani kuziandikisha ndege zao hizo na kupata leseni kutoka kwa mamlaka ya vyombo vya angani vya kiraia - ingawa hakuna mashirika ya mafunzo rasmi katika nchi hizi kuweza kupata leseni hizi. Nchini Rwanda, ndege za kigeni zinazorushwa kwa rimoti zinatakiwa kurushwa na raia wa Rwanda au biashara zinazomilikiwa na raia wa Rwanda.

Kanuni mpya ni ishara kwamba serikali nyingi za Kiafrika zinatambua  uwezo wa teknolojia ya ndege hizo, na wanaogopa kuwapa wananchi nguvu nyingi, anasema Miller. Na kuongeza kwamba kwa hali hiyo ya gharama za kujisajili, teknolojia ya ndege zinazorushwa kwa rimoti itabaki kumilikiwa na watu wachache wenye uwezo katika mataifa ya Afrika.

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Mhariri: Sekione Kitojo