Viwanja viwili vya ndege vyafungwa Ujerumani
25 Mei 2011Eneo la kaskazini la bara la Ulaya linatarajiwa kuingia katika mtafaruku mpya wa safari za anga leo kutokana na jivu linalotoka katika volcano nchini Iceland.
Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini Ujerumani imetangaza kuwa anga katika miji ya kaskazini ya Ujerumani litafungwa mapema leo Jumatano asubuhi kutokana na kiwango kikubwa cha majivu hewani kutokana na mlipuko wa volcano nchini Iceland. Maafisa wamesema jana Jumanne kuwa hakutakuwa na ndege itakayoruka ama kutua katika uwanja wa ndege wa Bremen, kuanzia saa 11 alfajiri leo ama katika uwanja wa ndege wa Hamburg, kuanzia saa 12 asubuhi leo Jumatano. Idara hiyo imesema kuwa inawezekana anga katika mji wa Berlin na Hannover likaathirika pia. Jana Jumanne, mamia ya safari za ndege katika anga la Uingereza zilifutwa wakati upepo ulisukuma mawingu ya jivu kutoka volcano ya Grimsvotn nchini Iceland na kuelekea kaskazini mwa Uingereza, hususan nchini Scotland.