1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ulaya yaipa Ukraine dola bilioni 5.5

Lilian Mtono
14 Machi 2024

Mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya yamekubaliana kuipatia Ukraine msaada zaidi wa kijeshi wa dola bilioni 5.5.

https://p.dw.com/p/4dUP8
Halmashauri ya Ulaya- Bendera ya Ukraine
Umoja wa Ulaya umekubaliana kuisaidia zaidi Ukraine kwa kuingezea msaada wa kifedha Picha: Lukasz Kobus/European Commission

Ubelgiji ambayo sasa ni mwenyekiti wa umoja huo imesema mabalozi kutoka mataifa hayo 27 wamekubaliana kimsingi juu ya mpango wa kusaidia upelekaji wa silaha nchini Ukraine.

Mchango huo utaingizwa kwenye mfuko unaoratibiwa na Umoja wa Ulaya wa European Peace Facility.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dymitro Kuleba ameyaita makubaliano hayo kuwa ya muhimu ya yaliyofikiwa kwa wakati muafaka.

Uamuzi wa kuongeza ufadhili ulicheleweshwa kwa miezi kadhaa kutokana na mvutano miongoni mwa wanachama juu ya namna utakavyotumika.

Brussels, Ubelgiji | Josep Borrell
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel amesema wataendelea kuisaidia Ukraine kwa namna yoyote ilePicha: John Thys/AFP/Getty Images

Makubaliano baada ya miezi kadhaa ya vuta nikuvute

Umoja wa Ulaya tayari umetoa yuro bilioni 6.1 kwenye mfuko huo ili kufidia sehemu ya gharama za silaha zilizotumwa na nchi wanachama kwenda Ukraine tangu ilipovamiwa na Urusi.

Soma pia:Biden kuhakikishia Poland msaada huku hofu ikiongezeka Kyiv

"Ujumbe uko wazi: tutaiunga mkono Ukraine kwa namna yoyote ile," mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell aliandika kwenye ukurasa wa X, iliyokuwa Twitter.

Mwezi Februari, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zilisaini mfuko wa msaada usio wa kijeshi wa yuro bilioni 50 (dola bilioni 54) ili kusaidia uchumi wa Ukraine hadi 2027. Fedha hizo zinajumuisha misaada na mikopo inayotoka kwenye bajeti ya Umoja wa Ulaya.