Vita vya kigaidi vimefika Ujerumani | Magazetini | DW | 06.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Vita vya kigaidi vimefika Ujerumani

Kwa kweli, leo ni mada moja hasa ambayo imegonga vichwa vya habari katika magazeti yote na pia kwenye kurasa za uchambuzi, yaani kukamatwa magaidi wanaotuhumiwa walipanga shambulio kubwa dhidi ya kituo cha jeshi la Marekani hapa Ujerumani.

Wasiwasi sasa ni mkubwa, kama tunavyoweza kusoma kutoka gazeti la “Tagesspiegel” la mjini Berlin:

“Vita vimefika kwetu katika maisha yetu ya kila siku. Kwa bahati nzuri tu, mashambulio yalizuiliwa. Lakini maonyo dhidi ya ugaidi ambayo yalitolewa tangu mwaka uliopita yalikuwa na msingi. Tena mafanikio katika kuwapeleleza magaidi na kuwakamata yanaweza kuutuliza wasiwasi kwa kiasi fulani tu, kwani tukio hilo linaonyesha vile ugaidi ulivyotukaribia.”

Mhariri wa “Stuttgarter Nachrichten” anajiuliza masuali tofauti akiandika:

“Je, mafanikio katika kuwakamata magaidi hao ni ishara kwamba idara za usalama zina uwezo na vifaa vya kutosha kupambana na ugaidi? Au je, mashambulio haya yaliyozuiliwa zaidi yanazusha hofu kwamba ugaidi umeenea mno?”

Magazeti mengine yanasifu kazi nzuri ya idara za usalama za nchini Ujerumani na zile za nje ambazo zimesaidia kuzuia mashambulio haya. Lakini wakati huo huo maonyo ni mengi. Mhariri wa “Offenbach-Post”, kwa mfano, anauliza:

“Kwa muda gani tutaweza kuyakimbia mashambulio? Jambo la kusikitisha ni kwamba mkasa huo unaonyesha kuwa pia kuna magaidi wa kienyeji na itakuwa vigumu kugundua nani anaweza kujiunga na makundi haya. Kwa hivyo, huu ni mwelekeo mpya wa kigaidi ambao ni changamoto kubwa kwetu sisi sote.”

Mhariri huyu alitaja juu ya Wajerumani wawili waliokuwa miongoni mwa waliokamatwa. Hilo jambo pia linazingatiwa na gazeti la “Tageszeitung” na limeandika:

“Wawili kati ya magaidi hao waliotengenezwa mabomu walikuwa Wajerumani waliosilimu. Haya yanaonyesha kuwa ugaidi wa kiislamu hauhusiani tu na wageni wanaohamia Ujerumani. Kwa hivyo haisaidii chochote kupinga uhamiaji ili kuzuia ugaidi nchini humu au kuzungumziwa tu suala la kuwaunganisha wageni katika jamii. Kwani yule ambaye anajiunga na kundi la Jihad hafanyi hivyo kwa sababu hafahamu lugha ya Kijerumani au kwamba hajapata kazi hapa nchini.”

Gazeti la “Die Welt”, kwa upande mwingine, linachambua kwa nini Ujerumani ni nchi inayowafaa magaidi:

“Wafuasi wa itikadi kali ya kiislamu wanazipendelea hasa nchi za Ulaya kupanga mashambulio haya, kwa vile nchi hizo wana uhuru mkubwa na ni rahisi kupata wafuasi wengine. Hasa Ujerumani inawapatia magaida nafasi nzuri za kujificha. Lazima nafasi hizo zipunguzwe. Kwa upande mmoja ni kupitia idara za ujasusi, na kwa upande mwingine ni kupitia jamii, hususan kutoka Waislamu wenzao. Hapa inabidi pia kuongeza juhudi za kuunda jamii ya pamoja.”

Na hatimaye ni gazeti la mjini Eßlingen ambalo linaonya kutoweka sheria kali zaidi kama anazozitaka waziri wa ndani wa Ujerumani. Gazeti limeandika:

“Haiwezekani kujikinga kabisa dhidi ya mashambulio ya kigaidi, si hapa Ujerumani wala kwengineko. Kwa hivyo, badala ya kuweka sheria kali zaidi kwa haraka, inapaswa kwanza kuchunguza ikiwa sheria zilizopo zimesaidia vya kutosha kuwakamata magaidi hao hivi karibuni.”

 • Tarehe 06.09.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHRu
 • Tarehe 06.09.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHRu