1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa G8,G5 na Afrika Wajadili Kilimo.

10 Julai 2009

Viongozi wa nchi 8 zilizoendelea kiviwanda duniani-G8 leo wanakutana na Viongozi wa Afrika kabla ya kutangazwa mapendekezo ya msingi ya kuboresha sekta ya Kilimo.

https://p.dw.com/p/IkyB
Viongozi wa G8,G5 na Afrika.Picha: AP

Viongozi wa nchi 8 zilizoendelea kiviwanda duniani-G8 leo wanakutana na Viongozi wa Afrika kabla ya kutangazwa mapendekezo ya msingi ya kuboresha sekta ya kilimo na kukabiliana na balaa la njaa.

Kutokana na mipango hiyo, wachambuzi wametumia msemo wa zamani unaonesema ``kumfundisha mtu kuvua samaki``

Wajumbe wanaohudhuria mkutano huo wa G8 wanasema Rais Barack Obama wa Marekani anatarajiwa kutangaza kiasi cha hadi dola bilioni 15 kwa ajili ya kuekezwa katika maendeleo ya kilimo. Biliioni 3 zitatoka Marekani.

Lengo la mpango huo ni kuwawezesha wakulima masikini walime chakula chao kutokana na kuboresha tija, shabaha ikiwa kuondokana na utaratibu wa kutoa msaada.

Huu ni mkakati mpya wenye lengo la kuleta uhakika wa chakula kwa kutambua kwamba uhaba wa chakula unatishia utengemavu wa kisiasa.

Viongozi wa nchi tajiri wanatarajiwa kutangaza mabadiliko ya kimsingi kwa kuzingatia njia wanazotumia katika kukabiliana na mabadiliko ya kimsingi yanayosababisha njaa duniani.

Kiasi cha fedha kilichotengwa kinatarajiwa kugawanywa kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kiongozi aliye mstari wa mble katika kuunga mkono jitihada hizo, waziri mkuu wa Uengereza, Gordon Brown, amesema wanataka kuionesha Dunia kwamba wanachukua hatua katika kukabiliana na njaa.

Mashirika ya misaada ya Kibinadamu yameonya kuwa mgogoro wa kiuchumi wa Kidunia umesababisha zaidi ya watu milioni 100 katika nchi zinazoendelea kuzidi kuzama katika dimbwi la umasikini, na hasa kukabiliwa na ukata wa chakula.

Belgien EU Gipfel Großbritannien Gordon Brown in Brüssel
Waziri Mkuu wa Uingereza British Prime Minister Gordon.Picha: AP

Kiasi hiki cha pesa kinachotarajiwa kutolewa sasa kitaelekezwa katika kununua mbegu bora, ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kuwafundisha wakulima njia bora na za kisasa za kilimo.

Hiví sasa nchi za kundi la G8 na zile zinazoinukia kiuchumi G 5 pamoja na viongozi kutoka Algeria, Angola, Misri, Libya, Nigeria na Senegal,Afrika ya Kusini pamoja na Umoja wa Afrika wameanza mazungumzo kuhusu kukabiliana na njaa.

Hatua hiyo inafuatia kauli ya nchi za G8 na G5 kusema zinataka kustawisha soko la kimataifa kabla ya mwaka ujao kumalizika, kuchachua maendeleo pamoja na kupunguza umasikini kwa nchi masikini.

Nchi za kundi la G8 zilizo mstari wa mbele mjini L'Aquila ni Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia,Urusi na Marekani.

Na kwa upande wa G5 kuna uwakilishi wa Brazil,China, India, Mexico na Afrika ya Kusini.

Lakini viongozi wengine kutoka nchi za Australia, Indonesia, Korea Kusini, Uhispania,Uturuki pamoja na Uholanzi pia wanaudhuria.

Mwandishi-Sudi Mnette DPAE

Mhariri-Othman Miraji