VFB Stuttgart-mabingwa wapya wa Ujerumani | Michezo | DW | 31.05.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

VFB Stuttgart-mabingwa wapya wa Ujerumani

VFB Stuttgart wametawazwa msimu huu mabingwa wapya wa Ujerumani baada ya kuwavua taji Bayern Munich.Waliikomea mchezo wa mwisho wa msimu huu E.cottbus mabao 2:1.

VFB Stuttgart ndio mabingwa wapya wa Ujerumani waliowavua taji msimu huu mabingwa mara kadhaa Bayern Munich.Kwa ushindi wa mabao 2:1 dhidi ya Energie Cottbus siku ya mwisho ya msimu wiki 2 zilizopita,Stuttgart ilitawazwa tena mabingwa wa Ujerumani wakizipiku timu za usoni msimu mzima-Werder Bremen ,Schalke na Bayern Munich.

Kusema kweli, hakuna alietazamia kuwa Stuttgart ingeibuka mabingwa wa Ujerumani pale msimu huu ulipoanza .Wengi wakitazamia ama Bayern Munich kutetea taji lao au makamo-bingwa werder Bremen kuwavua taji.Schalke pia ilipewa nafasi ya kutoroka na taji na hata Hamburg.Stuttgart la hasha.Lakini kama wasemavyo mpira unadunda.

Baada ya firimbi ya mwisho kulia na Stuttgart imeizaba Cottbus mabao 2:1 ripota uwanjani alisimulia hivi:

“Akiwa na fahari kubwa kabisa Fernando Meira ame nyanyua hapo kombe la dhahabu la ubingwa.Hii ni ajabu kabisa,kwani hakuna alietazamia kuwa VFB Stuttgart kabla kuanza msimu huu ingezusha maajabu haya.Lakini imefanya kila kitu barabara sawa na kocha na meneja wao Armin Veh na Horst Held.”

Ni wazi kabisa meneja Horst Held na kocha Armin Weh, ndio baba wa ushindi wa Stuttgart msimu huu.Stuttgart, ikicheza imara mara kwa mara .Ikionesha mbinu madhubuti na ikipasiana pasi maridadi ajabu- pasi fupi na za kuonana na ikizidi kuzikosha nyoyo za mashabiki wake huku ikikusanya kikapuni mwake point zaidi na zaidi na mwishoe, ikastahiki kutwaa ubingwa.

Kocha Armin Weh asema:

“Hakuna aliewatazamia kutwaa ubingwa.Kwani tuna timu mpya katika Ligi.Kwamba timu yetu ni kali hii nilitambua wakati wa mazowezi ya wiki 6 kabla kuanza msimu.Kutokana na mchezo wetu msimu mzima tumestahiki kabisa ubingwa.”

Asema kocha wa Stuttgart.Aliongeza kusema zaidi kwamba kwa ushindi wa Stuttgart,timu changa kabisa ya Ligi imevaa taji na nani aliedhani hivyo baada ya kuuzwa kwa wachezaji staid kama akina Kevin Kuranyi,Henkel na weenzake ?

Mchango mkubwa kabisa katika ushindi wa mabingwa Stuttgart ametoa meneja Horst Held.Kwani ni mkono wake mzuri ulionunua mastadi waliwika.Pia aliweka imani kubwa kwa kocha wake Armin Veh katika kipindi cha msukosuko.

Ubingwa wa Stuttgart msimu huu ni 5 wa taji la Bundesliga.Meneja wa Stuttgart Horst Held anaeleza kuwa kila mmoja alitoa mchango wake katika wadhifa alionao-ama wachezaji uwanjani,makocha au wale ambao hawakuingizwa katika timu.kila mmoja alivuta kamba upandewake.

Ushindi wa mwisho wa taji la ubingwa kwa Stuttgart ulikuwa miaka 15 nyuma na enzi zile nahodha alikuwa guido Buchwald.Kuhusu ubingwa wa mwaka huu,Buchwald anasema : “Stuttgart msimu huu ilicheza kwa nguvu kabisa tena mechi zote 34 na kwahivyo imestahiki kuvaa taji.”

Mnamo miaka 4 iliopita imekuwa desturi mshindi wa taji la Bundesliga kuvaa pia taji la kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB Pokale).Jumamosi iliopita, Stuttgart ilitaka kutoroka pia na kombe hilo katika uwanja wa olimpik wa Berlin.Lakini, majirani zao wa kusini,Nüremberg, waliwazima na wakalichukua wao kombe hilo baada ya kuwachapa mabao 3-2 uliporefushwa mchezo.

Sasa VFB Stuttgart ndio itakayoiwakilisha Ujerumani msimu ujao katika champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya na sio mabingwa mara kadhaa Bayern Munich waliomaliza nafasi ya 4 safari hii na watahamia kombe la UEFA.Stuttgart itatakapia kuvuma ikiwa si kutamba pia katika champions League msimu ujao na kufika alao mbali zaidi kuliko Bayern munich msimu huu.

 • Tarehe 31.05.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHc6
 • Tarehe 31.05.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHc6