Matokeo ya mwanzo yanaashiria kuwa Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan na mpinzani wake mkuu Muhammadu Buhari huenda wakawa na ushindani mkubwa baada ya uchaguzi wa rais uliofanyika Jumamosi(16.04.2011.
Ramani ya Nigeria
Duru zinaeleza kuwa uchaguzi huo umefanyika katika mazingira ya kuaminika ikilinganishwa na uliotokea awali. Kulingana na matokeo hayo ya mwanzo, Goodluck Jonathan anaongoza katika eneo la kusini mwa Nigeria lililo na Wakristo wengi ukiwemo pia mji wa Lagos.
Wapiga kura kwenye foleni, Nigeria: Zaidi ya milioni 70 wamesajiliwa
Kwa upande mwengine, mpinzani wake mkuu Muhammadu Buhari anaongoza katika majimbo ya kaskazini kuliko na Waislamu wengi. Hali inaripotiwa kuwa ya wasiwasi katika eneo la kaskazini wakati ambapo shughuli ya kuhesabu kura inaendelea. Kwa mujibu wa sheria, ili mgombea atangazwe mshindi lazima apate wingi mkubwa na robo ya kura katika theluthi mbili ya majimbo yote 36. Zaidi ya watu milioni 73 walisajiliwa kushiriki katika uchaguzi huu unaofanyika kwenye zaidi ya vituo 120,000 vya kupigia kura kote nchini Nigeria. Matokeo ya mwisho yanatazamiwa kutangazwa baada ya siku kadhaa.