1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na China zapinga Azimio la Ufaransa dhidi ya Syria

22 Mei 2014

Jeshi la Syria limewatimua waasi waliokuwa wakiizingira jela ya mji wa Aleppo tangu mwaka mmoja uliopita.Wakati huo huo Urusi na China zimetumia kura za turufu kuzuwia azimio la baraza la usalama dhidi ya Syria

https://p.dw.com/p/1C4lX
Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa lakutana kupiga kura kuhusu azimio dhidi ya SyriaPicha: Reuters

Ushindi huo wa vikosi vya jeshi la serikali umejiri masaa machache kabla ya baraza la usalama la umoja wa mataifa kulipigia kura azimio lililowasilishwa na Ufaransa kutaka korti ya kimataifa ichunguze madai ya uhalifu wa vita nchini Syria.Kwa mara ya kwanza kabisa Urusi na China zimetumia kura zao za turufu kuupinga azimio hilo.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa bibi Samantha Power anasema licha ya kukataliwa azimio hilo, nchi yake haitopakata mikono hadi wahanga wa uhalifu nchini Syria wanatendewa haki

Jela kuu ya Aleppo yakombolewa

Jeshi la Syria likisaidiwa na vkosi vya ulinzi wa taifa-FDN,wanamgambo wa Hisbollah wa kutoka Libnan na wapiganaji wengineo wa kiarabu limefanikiwa kuivunja ngome ya waasi waliokuwa wakiizingira kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa jela kuu ya mjini Aleppo-kaskazini ya Syria.

Syrien Gefängnis in Aleppo
Jela kuu ya Aleppo kaskazini ya SyriaPicha: AFP/Getty Images

Mkurugenzi wa shirika linalosimamia masuala ya haki za binaadam nchini Syria,lenye makao yake makuu nchini Uingereza Rami Abdel Rahmane amethibitisha ripoti hizo.Akizungumza na waandishi habari bwana Rami Abdel Rahman amesema vifaru viliingia katika uwanja wa jela hiyo na risasi kufyetuliwa mtindo mmoja kabla ya vikosi vya kawaida vya jeshi kuwasili katika eneo hilo.Watu 50 wanasemekana wameuwawa miongoni mwa waasi.Hasara upande wa vikosi vya serikali bado haijulikani.Waasi waliokuwa wakiizingira jela hiyo walikuwa wamepania kuwafungua wafungwa elfu nne wengi wao wa makosa ya jinai.

Damascus inatarajia haali kama ile ya Homs

Ushindi wa jeshi la Syria katika eneo hilo la kaskazini unapelekea kufungwa njia muhimu ya kupatiwa misaada waasi kutoka maeneo wanayoyadhibiti na lile linalopakana na Uturuki.

Homs Rebellen Evakuierung 09.05.2014
Waasi walipolazimika kuuhama mji wa Homs mapema mwezi huu wa Mei 2014Picha: Reuters

Kwa mujibu wa gazeti linaloelemea upande wa serikali,Al Watan, ushindi wa vikosi vya jeshi la serikali "utafungua ukurasa mpya katika medani ya mapigano.Ushindi huo utasaidia kuimarisha udhibiti wa mji huo na hasa katika mitaa inayokaliwa na makundi ya watu wenye silaha na kulazimisha kufikiwa makubaliano sawa na yale yaliyofikiwa Homs".

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu