1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

UN: Watu milioni 5 wakabiliwa na baa la njaa Sudan

Zainab Aziz
16 Machi 2024

Umoja wa Mataifa umesema Wasudan milioni tano wanakabiliwa na uhaba wa chakula unaoweza kuwatumbukiza kwenye baa la njaa katika miezi michache ijayo.

https://p.dw.com/p/4dnpy
Wakimbizi wa ndani nchini Sudan
Wakimbizi wa ndani nchini Sudan wakipata msaada wa matibabu kutoka kwa madaktari wasio na mipakaPicha: Mohammad Ghannam/MSF/REUTERS

Hali hiyo ni kutokana na vita vya karibu mwaka mzima nchini Sudan kati ya majenerali hasimu vinavyoendelea kuisambaratisha nchi hiyo.

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa pande zinazohasimiana kuruhusu usafirishaji wa misaada ya kibinadamu ili kulikabili janga la njaa. Pande hizo ni jeshi linalomuunga mkono kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani, Jenerali Mohamed Hamdan Daglo, kiongozi wa kundi la wanamgambo walioasi la RSF.

Soma pia: Jeshi la Sudan lakataa kusitisha mapigano mwezi wa Ramadhani

Jill Lawler, mkuu wa idara ya dharura wa shirika laUmoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF, nchini Sudan amesema ipo hifadhi ya kutosha ya misaada katika Bandari ya Sudan, lakini tatizo ni namna ya kuisafirisha misaada hiyo kwenda kwa watu wanaoihitaji.

Mratibu wa misaada wa UN atoa tahadhari

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu Martin Griffiths ametahadharisha kuwa, Wasudan milioni 18 tayari wanakabiliwa na uhaba wa chakula kiwango hicho kikiwa rikodi wakati wa msimu wa mavuno.

Griffiths ameeleza kuwa, karibu watoto 730,000 nchini humo, ikiwa ni pamoja na zaidi ya watoto 240,000 katika jimbo la Darfur, wanaelezwa kuwa na utapiamlo mbaya.

Martin Griffiths Mratibu wa wa misaada ya kibinadamu wa UN
Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu Martin GriffithsPicha: Martial Trezzini/dpa/Keystone/picture alliance

Kulingana na waraka wa Umoja wa Mataifa ulioonekana na shirika la habari la AFP, vita hivyo vya tangu mwezi Aprili mwaka jana vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, kuharibu miundombinu na vimeathiri Uchumi wa Sudan.

Umoja wa Mataifa umeomba dola bilioni 2.7 mwaka huu kwa ajili ya kuwezesha kupatikana misaada kwa watu wa Sudan lakini umesema umepokea asilimia tano tu ya fedha hizo hadi kufikia sasa.

Waziri wa fedha wa Sudan Kusini afutwa kazi

Wakati huo huo Rais wa Sudan KusiniSalva Kiir amemfuta kazi waziri wake wa fedha bila ya kutoa sababu, ingawa hatua hiyo imechukuliwa huku kukiwa na ongezeko la mfumuko wa bei na kushuka kwa kasi thamani ya fedha za nchi hiyo dhidi ya dola ya Marekani.

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Pauni ya Sudan Kusini ilipoteza karibu nusu ya thamani yake dhidi ya dola ya Marekani hali iliyochochea kupanda kwa bei ya vyakula na mahitaji mengine muhimu.

Kufukuzwa kwa waziri, Bak Barnaba Chol, kulitangazwa katika televisheni ya taifa siku ya Ijumaa.

Chol, mwenye umri wa miaka 43, na mshirika wa rais Salva Kiir, aliteuliwa kuwa waziri wa fedha mwezi Agosti mwaka uliopita na alifanya mageuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuondoa majina ya wafanyakazi hewa serikalini na pia kuziba njia za kuvujisha mapato ya serikali.

Rais Kiir amemteua Awow Daniel Chuong, waziri wa zamani wa mafuta ya petroli, kuwa waziri mpya wa fedha.

Kadiri mzozo wa uchumi wa nchini Sudan Kusini unavyozidi kuongezeka, baadhi ya watumishi wa umma hawajapata mishahara kwa muda wa miezi sita sasa.

Vyanzo: AFP/RTRE