1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Mizozo huwauwa na kuwaumiza watoto 12,000

Bruce Amani
30 Julai 2019

Zaidi ya watoto 12,000 waliuawa na kujeruhiwa katika mizozo ya kivita mwaka jana. Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imesema idadi kubwa ya vifo hivyo vilitokea Afghanistan, Palestina, Syria na Yemen

https://p.dw.com/p/3MxD3
Syrien Hilfslieferungen in Ghuta
Picha: Getty Images/AFP/A. Doumany

Aidha ripoti hiyo imesema vifo hivyo na majeraha ni miongoni mwa zaidi ya matukio 24,000 ya ukiukaji mkubwa dhidi ya watoto yaliyothibitishwa na Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kutumikishwa watoto jeshini kama wapiganaji, dhuluma za kingono, utekaji na mashambulizi shuleni na hospitalini.

Ripoti ya kila mwaka ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa Baraza la Usalama kuhusu Watoto katika Mizozo ya Vita inasema ukiukaji unaofanywa na makundi ya wapiganaji upo pale pale lakini kuna ongezeko la matukio ya ukiukaji unaofanywa na wanajeshi wa serikali na kimataifa ikilinganishwa na mwaka wa 2017.

Orodha mbaya inayosubiriwa kwa hamu kutolewa na katibu mkuu ya nchi ambazo zimefanya ukiukaji mkubwa wa haki za watoto wakati wa migogoro inaonekana kutokuwa na tofauti kubwa sana na ya mwaka jana, kitu kinachoyakasirisha makundi kadhaa ya haki za binaadamu.

Human Rights Watch na Watchlist on Children and Armed Conflict, shirika la utetezi la kimataifa, yamekasirishwa na kubakishwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kwenye orodha ya wahusika ambao wameweka hatua za kuwalinda watoto, yakitaja ongezeko la vifo vya watoto vinavyosababishwa na wanajeshi wa serikali na wanajeshi wa muungano nchini Yemen.

Jemen Konflikt l UN Generalsekretär Antonio Guterres
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: picture alliance/Photoshot/X. Jinquan

Afghanistan inaongoza orodha hiyo ambapo watoto 3,062 waliripotiwa kuuawa mwaka wa 2018, nchini Syria mashambulizi ya angani, mabomu ya mapipa na ya mabomu ya kutapakaa yaliwauwa na kuwajeruhi vijana 1,854 na nchini Yemen, watoto 1,689 waliuawa kutokana na mapigano

Katika mzozo wa Israel na Wapalestina, Umoja wa Mataifa umesema watoto wengi waliuliwa mwaka wa 2018 huku kukiwa na idadi iliyothibitishwa ya watoto 59 wa Kipalestina na 2,756 wakajeruhiwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pande zinazohasimiana Somalia ziliwaingiza jeshini na kuwatumikisha watoto 2,300, wengine wakiwa na umri mdogo kabisa wa miaka nane. Wanamgambo wa al-Shabaab waliongeza kwa kiasi kikubwa usajili wao kwa kuwaingiza jeshini vijana 1,865.

Nigeria ilikuwa katika nafasi ya pili, ambapo watoto 1,947 waliingizwa vitani, wakiwemo baadhi waliotumiwa kama walipuaji wa kujitoa mhanga.

Somalia pia ilikuwa na idadi kubwa ya takwimu zilizothibitishwa za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto, ambapo visa 331 viliripotiwa mwaka wa 2018, ikifuatwa na Congo na visa 277 ijapokuwa katibu mkuu anasema matukio bado hayaripotiwi sana hasa kuwahusu wavulana kwa sababu ya unyanyapaa. Somalia pia ilikuwa na idadi kubwa ya watoto waliotekwa nyara mwaka jana – 1,609.

Guterres amesema maelfu ya watoto pia waliathiriwa na mashambulizi 1,023 yaliyothibitishwa kufanywa kwenye shule na hospitali mwaka jana. Nchini Syria, kulikuwa na mashambulizi 225 kwenye shule na vituo vya afya mwaka wa 2018, ikiwa ndio idadi kubwa kabisa tangu kuanza kwa vita mwaka wa 2011. Aidha kumekuwa na ongezeko la mashambulizi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Colombia, Libya, Mali, Nigeria, Somalia, Sudan na Yemen.