UN kupiga kura kuhusu suala la Jerusalem
18 Desemba 2017Misri hapo jana iliomba kupigwa kura hiyo, siku moja baada ya kuwasilishwa azimio hilo ambalo linatazamiwa kupingwa na Marekani kupitia kura ya turufu.
Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence atazuru Jerusalem siku ya Jumatano, akijitumbukiza katika mzozo wa moja kati ya suala lenye utata kabisa katika mzozo kati ya Wapalestina na Israel. Israel ilichukua udhibiti wa sehemu ya mashariki mwa mji huo katika vita vya mashariki ya kati mwaka 1967 na inaliona eneo lote la mji wa Jerusalem kuwa mji ambao haukugawanyika.
Ukraine, mshirika wa Marekani katika baraza la usalama, hata hivyo imeelezea wasiwasi kuhusu uamuzi huo na kuomba kupewa muda wa ziada. Baraza hilo litaandaa kiikao cha faragha leo ili kujadili mswada wa azimio hilo kabla ya kupigiwa kura.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alielezea matumaini kuwa Uturuki hivi karibuni huenda ikafungua ubalozi katika Jerusalem Mashariki, wakati akilaani kwa mara nyingine hatua ya Trump kuutambua mji huo kuwa mji mkuu wa Israel.
Mswada huo wa azimio unatoa wito kwa nchi zote kujizuwia kufungua balozi zao mjini Jerusalem, ukiakisi wasiwasi kwamba serikali nyingine zinaweza kufuata kile Marekani ilichofanya.
Mswada huo unataka kwamba mataiafa yote wanachama kutotambua hatua yoyote ambayo itakwenda kinyume na maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu hadhi ya mji huo. Maazimio kadhaa ya Umoja wa Mataifa yanaitaka Israel kujiondoa kwenye maeneo iliyoyatwaa wakati wa vita yam waka wa 1967 na yanasisitiza kuhusu haja ya kusitisha kukaliwa ardhi hiyo.
Wapalestina walitaka azimio lenye maneno makali ambalo lingeutaka utawala wa Marekani kuufuta uamuzi wake, lakini nakala ya mwisho ilipunguzwa makali ili kutafuta uungwaji mkono wa kutosha.
Huku wakiungwa mkono na nchi za waislamu, Wapalestina wanatarajia kuigekia hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa kuidhinisha azimio linalopinga uamuzi wa Marekani, ikiwa, kama inavyotarajiwa, hatua hiyo itapingwa na Marekani katika Baraza la Usalama.
Kando na Marekani, Uingereza, China, Ufaransa na Urusi zinaweza kutumia kura a turufu kupinga azimio lolote linalowasilishwa katika baraza hilo, ambalo linahitaji kura tisa ili kuidhinishwa.
Wakati hayo yakijiri, ndege za kijeshi ka Israel zimekishambulia kituo kimoja cha Hamas kaskazini mwa Ukanda wa Gaza mapema leo, saa chache tu baada ya maroketi mawili yaliyofyatuliwa kutokea eneo la Wapalestina kupiga kusini mwa Israel. Wanamgambo katika upande wa Wapalestina wamekuwa wakifyatua maroketi kuelekea Israel tangu Trump alipotoa tangazo lake lenye utata.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo