1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya watafuta muafaka

Maja Dreyer20 Juni 2007

Katiba hamna tena, lakini kuna mkataka mpya wenye marekebisho. Haya basi ni makubaliano viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya waliyafikia. Ila tu nchi moja yaani Poland bado inakataa kukubali masharti yote hususan lile la namna ya kupiga kura. Kuanzia Alhamisi viongozi wa nchi zote 27 wanachama wa Umoja huu wanaanza mkutano wao wa siku mbili mjini Brussels ambapo watajaribu kutafuta njia ya muafaka. Nini basi misimamo ya nchi wanachama?

https://p.dw.com/p/CHCQ
Picha: Toms Grinbergs

Baada ya Wafaransa na Waholanzi kupinga katiba mpya ya Umoja wa Ulaya katika kura za maoni mwaka 2005, mradi huo umeshindwa kutekelezeka. Mbinu sasa ni kuwa na mkataba mpya wa msingi ambao utachukua nafasi ya mkataba wa Umoja wa Ulaya uliotiwa saini mwaka 2000 mjini Nizza, Italy. Serikali ya Ujerumani, hata hivyo, inataka kutumia baadhi ya masharti yaliyoandikwa katika mswada wa katiba ambao uliidhinishwa na nchi 18 kati ya nchi zote 27 wanachama wa Umoja huu. Moja ya masharti haya ni lile linalohusu namna ya kupiga kura ambayo itakuwa rahisi kuliko zamani.

Badala ya kuhesabu idadi ya aina tatu, yaani mataifa yenyewe, nguvu za kura zao pamoja na asilimia ya idadi ya watu, siku za usoni wingi wa kura utakuwa ni zaidi ya asimilia 55 ya mataifa wanachama pamoja na zaidi ya asilimia 65 ya idadi ya watu wa Ulaya yote. Lengo la utaratibu huu ni kuzuia idadi ndogo ya nchi hizi kuweza kusimamisha mradi fulani. Miaka mitatu iliyopita, serikali zote za nchi wanachama zilitia saini makubaliano juu ya wingi huu wa aina mbili. Ndiyo sababu, Ujerumani kama mwenyekiti imeshtushwa sana kutokana na kwamba Poland sasa inataka kubadilisha tena utaratibu huu.

Hoja ya Poland ni kwamba haitaka mkataba wa Nizza ukerebishwe kwa sababu katika mkataba huu Poland inanufaika zaidi. Kwa hivyo, Poland inataka nguvu za nchi kubwa kama Ujerumani yenye wakazi wengi zipunguzwe. Kati ya nchi 27, 25 zilipinga pendekezo hilo. Nchi ya Czechia peke yake ilisema itaiunga mkono Poland. Licha ya majaribio mengi ya wajumbe wa Umoja wa Ulaya kuishawishi Poland, waziri mkuu Jaroslaw Kaczynski alionya juu ya kukadiria nia ya Poland kupigania maslahi yake. Kwenye televisheni ya taifa, Kaczynski alisema: “Tunakwenda Brussels kwa nia ya kupigania maslahi yetu. Licha ya kuwa hali ni ngumu, bado tuna fursa. Pengine tutachukua uamuzi mzito, kwani kura ya turufu ni uamuzi mzito.”

Si tu Poland lakini ambayo inataka mtakaba mpya urekebishwe tena. Uingereza, Ufaransa na Uholanzi pia zimetoa maombi juu ya mkataba huu. Kwa mujibu wa serikali ya Ujerumani kama mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya kwa sasa hivi, maombi haya yataweza kupata muafaka. Uingereza inataka kutolazimisha kutokana na maamuzi ya pamoja fulani ya Umoja wa Ulaya. Sheria za Kiingereza zinahitajika zisiguswe, ama sivyo itabidi Waingereza pia wapige kura juu ya mkataba. Matokeo ya kura hiyo lakini hayajulikani, ila tu kwamba Waingereza wana wasiwasi juu ya Umoja wa Ulaya.

Uholanzi haitaki Umoja wa Ulaya uwe na usemi zaidi katika sera za sheria na mambo ya ndani. Wala haitaki kuwepo bandera au wimbo wa Umoja wa Ulaya kama alama za kitaifa. Ufaransa inataka mkataba usiwe na sheria za msingi, bali uhusu mageuzi ya usimamizi tu.

Licha ya misimamo tofauti, waziri mdogo wa Ujerumani anayehusika na masuala ya Ulaya, Günter Gloser bado ana matumaini mazuri, akisema: “Mshikamano hauhakikishi muelekeo mmoja tu. Bali inabidi kukubaliana. Hatuwezi kuzingatia maombi ya nchi moja, mbili, tatu tu. Na hatuwezi kuzungumzia upya kila suala. Kwa hivyo nina matumaini fulani kwamba tutaweza kukubaliana.”

Matokeo basi yatajulikana Ijumaa ambapo mkutano huu wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakapomalizika.