1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Umoja wa Ulaya walaani ghasia zinazoendelea huko Darfur

13 Novemba 2023

Umoja wa Ulaya umeonya na kuelezea wasiwasi wake kuhusu hatari ya kutokea mauaji mengine ya kimbari kama yale yalitokea kati ya mwaka 2003 hadi 2008 Kutokana na kuongezeka kwa ghasia katika jimbo la Darfur nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/4Yk0L
Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell
Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Josep BorrellPicha: Press Office, Albania Premiership

Vita vikali vilivyoibuka tangu mwezi April kati ya Jeshi laSudan na kundi la wanamgambo la RSF,  vimesababisha uharibifu na ukosefu wa utulivu na amani baada ya mapigano hayo kuendelea kwa muda kwenye ukanda huo wa Magharibi. 

Ripoti zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zimeeleza kuwa watu wapatao milioni 4.8 hawana makazi ndani ya Sudan  na wengine milioni 1.2 wamelazimika kukimbilia nchi jirani.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya washutushwa na mauaji ya raia 1,000 Darfur

Taarifa ya Umoja wa Ulaya ilisema "kulikuwa na ripoti za mashahidi wa kuaminika kuwa zaidi ya watu elfu moja wa kabila la Masalit waliuawa huko Ardamta, Darfur Magharibi, katika muda wa siku mbili tu, wakati wa mashambulizi makubwa yaliyofanywa na kundi la wanamgambo la (RSF) na wanamgambo wake washirika.

Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amenukuu ripoti zilizotolewa na mashahidi na kusema ukatili unaoendelea unaonekana kuwa sehemu ya matukio makubwa zaidi. 'Kampeni ya utakaso ya kikabila' inayoendeshwa na RSF kwa lengo la kutokomeza jamii ya Wamasalit wasio Waarabu kutoka Darfur Magharibi, inaongezeka kwa kasi tangu lilipofanyika vurugu kubwa ya kwanza mwezi Juni. 

Wanamgambo wa RSF
Wanamgambo wa RSFPicha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Borell pia ameongeza kusema Jumuiya ya kimataifa haiwezi kufumbia macho mambo yanatokea Darfur na kuruhusu mauaji mengine ya kimbari kutokea kwenye ukanda huo.

RSF na wanamgambo washirika wadaiwa kuendesha dhidi ya jamii ya Masalit

Wiki iliyopita RSF ilisema kuwa imechukua udhibiti wa ngome kuu ya jeshi katika mji mkuu wa Darfur Magharibi wa El Geneina.

Shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa kati ya Aprili na Juni mwaka huu, kundi la wanamgambo la RSF na wanamgambo washirika wa Kiarabu waliendesha  mashambulizi yaliyoilenga jamii ya Masalit, kabila kubwa la El Geneina, vita iliyopambishwa moto na jeshi la Sudan.

El Geneina Darfur Magharibi
El Geneina Darfur Magharibi Picha: Str/AFP

Kwa upande wao viongozi wa makabila ya Kiarabu wamekanusha kuhusika katika kampeni hiyo iliyoitwa utakaso wa kikabila huko El Geneina. Kundi la wanamgambo la RSF pia limewahi kukanusha tuhuma hizo na kusema hawakuhusika katika kile walichokiita migogoro ya kikabila.

Umoja wa Ulaya ulisisitiza kuwa pande zinazozozana za Sudan "zina jukumu la kuwalinda raia". pia ulisema ilikuwa inafanya kazi na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuweka kumbukumbu za ukiukaji katika kuhakikisha wanawajibika.