1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

RSF inatuhumiwa kufanya mauaji katika jimbo la Darfur

10 Novemba 2023

Miili ya watu waliovalia sare za jeshi imetapakaa mji mkuu wa Sudan, Khartoum, kufuatia kile mashuhuda walichosema ni matokeo ya mapigano ya hapo jana kati ya vikosi vya Jeshi na kundi la wanamgambo walioasi wa RSF.

https://p.dw.com/p/4YfMp
Kundi la wanamgambo la RSF
Kundi la wanamgambo la RSFPicha: Ashraf Shazly/AFP

Shirika la Habari la AFP wamezungumzia hali ya kutisha mjini Khartoum ambako maiti zimetapakaa mitaani hususani katikati mwa mji huo mkuu. 

Shuhuda mmoja aliyezungumza kwa njia ya simu na Shirika la habari la AFP kutoka mji pacha wa Khartoum wa Omdurman amesema miili ya watu hao waliovalia gwanda za jeshi,  imeonekana baada ya mapigano makali yaliyoibuka hapo jana. 

Soma zaidi: Mauaji ya kikabila yaripotiwa kuongezeka Darfur Magharibi

Mashuhuda wengine wamesema kombora moja liliinguka kwenye hospitali ya Al-Nau kaskazini mwa Omdurman. Hicho ndiyo kituo pekee cha matibabu kinachofanya kwenye eneo hilo. Kombora hilo limesababisha kifo cha mwanamke mmoja.

Majenerali wanaohasimana Abdel Fattah  al-Burhan na Mohamed Hamdan Daglo
Majenerali wanaohasimana Abdel Fattah al-Burhan na Mohamed Hamdan DagloPicha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Tangu mwezi Aprili, vikosi vinavyoongozwa na Abdel Fattah al-Burhan vimekuwa kwenye mapigano na kikundi cha wanamgambo cha (RSF) kinachoongozwa na makamu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Daglo.

Mapigano makali yameshababisha umwagaji mkubwa wa damu na yametanda kwenye mji mkuu, Khartoum na maeneo mengine hususani jimbo la magharibi la Darfur ambapo kundi la wanamgambo la RSF, limedai kudhibiti maeneo karibu yote isipokua mji mmoja ulio karibu na Darfur. Pia kumekua na hofu ya kuongezeka kwa mauaji ya kikabila kufuatia kukatika kwa mawasiliano.

Soma zaidi: RSF wachukuwa udhibiti wa Kordofan Magharibi

Naibu Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa huko Darfur, Toby Harward kupitia ukurasa wake wa X ameandika, 'mamia kwa maelfu ya raia na watu waliokimbia makazi yao sasa wako katika hatari kubwa huko El Fasher, Darfur Kaskazini, na hali ya usalama inazidi kudorora,

Kiongozi huyo amebainisha uwepo wa uhaba wa chakula na maji. Kiongozi huyo pia ameongezea, ikiwa kundi la wanamgambo la RSF na jeshi la Sudan wataendelea kupigania udhibiti wa mji, waathiriwa zaidi watakua ni raia.

Wakimbizi wa nchini Sudan
Wakimbizi wa nchini SudanPicha: Marie-Helena Laurent/WFP/AP/picture alliance

Ubalozi wa Marekani mjini Khartoum umesema 'umesikitishwa sana na ripoti zinazotolewa na watu walioshuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na RSF na wanamgambo washirika. Pia ubalozi huo umejumuisha mauaji yaliyofanywa huko Ardamata yaliyowalenga viongozi na wanachama wa jumuiya ya Masalit.

Baraza la utawala la Sudan, liliripoti kifo cha kiongozi wa kabila la Masalit Mohammad Arbab, pamoja na mtoto wake wa kiume na wajukuu zake nane likisema 'kiongozi huyo aliuawa na kundi la wanamgambo la RSF baada ya kushambulia makazi ya raia huko Ardamata'.

Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa, zimeainisha kuwa tangu kuzuka kwa mapigano hayo mnamo Aprili 15 zaidi ya watu 10,000 wameuawa nchini Sudan, na takribani watu milioni sita wameyahama makazi yao huku wengi zaidi wakikimbilia nje ya mipaka ya nchi hiyo.

Soma zaidi: Maafisa wa UN waonya kuongezeka kwa mateso ya raia wa Sudan

Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, wakimbizi waliowasili taifa jirani la Sudan Kusini wameongezeka kwa asilimia 50 kati ya Septemba na Oktoba, ambapo ametaja kuwa ongezeko hilo la watu wapatao 366,000 waliokimbilia Sudan Kusini tangu kuanza kwa vita hivyo huenda ikapelekea Sudan Kusini kuelemewa katika utoaji huduma za kijamii.  

Nalo Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) katika ripoti yake limeeleza kuwa kati ya Novemba 4 na 5 huko El Geneina watu takribani 700 waliripotiwa kuuawa, huku 100 wakijeruhiwa na wengine 300 hawajulikani walipo, kufuatia mapigano kati ya Jeshi la Sudan kundi la wanamgambo la RSF.