1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wathibitisha mamluki wa Urusi wapo Libya

Tatu Karema
7 Mei 2020

Umoja wa mataifa wamesema Jumatano kuwa mamluki wa kundi la Wagner la Urusi linaloonekana kuwa karibu na Rais Vladmir Pitin wanapigana nchini Libya, kwa mujibu wa ripoti ya wataalamu kuhusu marufuku ya silaha Libya.

https://p.dw.com/p/3bug2
Libyen GNA-Kämper gegen LNA
Picha: Imago-Images/A. Salahuddien

 

Hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kuthibitisha madai yaliotolewa mara ya kwanza katika vyombo vya habari vya Marekani kwamba kundi hilo linamuunga mkono mbabe Khalifa Haftar. Urusi imekanusha kuhusika kupeleka kundi hilo.

Kundi la Wagner ni kampuni ya kibinafsi ya ulinzi na maelfu ya wanakandarasi wake wanaaminika kuhusika katika mizozo ya kimataifa kutoka Syria hadi Ukraine hadi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Afisa mmoja mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba kundi hilo ni ‘’ chombo cha sera za ikulu ya rais ya Urusi’’ nchini Libya.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa jopo hilo limetambua uwepo wa maafisa wa kijeshi wa kibinafsi kutoka kundi la ChVK Wagner nchini Libya tangu Oktoba 2018," kwa mujibu wa wajumbe kadhaa waliozungumza na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotambulishwa kwasababu nyaraka hiyo bado haijatolewa hadharani.

Majukumu ya kundi la Wagner

Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa kundi hilo limekuwa likitoa usaidizi wa kiufundi kwa kufanyia marekebisho magari ya kijeshi , kushiriki katika operesheni za kijeshi na kujihusisha na operesheni za kutoa shinikizo

Libyen General Khalifa Haftar
Mbabe wa kivita nchini Libya, Khalifa HaftarPicha: Reuters/C. Balta

Ripoti hiyo pia imesema kuwa kundi hilo pia linahusika katika ‘’ majukumu ya kitaalamu ya kijesi kama vile maafisa wa kuelekeza silaha kwenye maeneo yaliolengwa  na kutoa mbinu za kitaalamu za kilektroniki za hatua za kujibu mashambulizi na pia kupeleka makundi ya maafisa hodari wa mashambulizi ya risasi.

‘’Kupelekwa kwa kundi hilo kumechangia kama njia bora ya kuongezeka’’ kwa kikosi cha Haftar.

Wataalamu hao wanasema kuwa hawakuweza kuthibitisha idadi kamili ya mamluki hao wa kundi la Wagner nchini Libya lakini wamekadiria kuwa kati ya 800 na 1200.

Ripoti iliyowasilishwa tarehe 24 mwezi Aprili kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa hata hivyo imesema kuwa kuna hofu kati ya kundi la Wagner na uongozi wa Haftar.

Masuala ya ziada katika ripoti hiyo

Ripoti hiyo ni mwendelezo wa ripoti ya mwaka jana ya jopo hilo la wataalamu kutoka mwezi Desemba ambayo ilikuwa imetambua uwepo wa makundi ya kujihami ya kigeni kutoka Chad na Sudan katika mzozo huo lakini haikutaja kundi la Wagner.

Pia inathibitisha uwepo wa kampuni nyingine  ya kibinafsi ya ulinzi kutoka Urusi inayojulikana kama kundi la Rossiskie System Bezopasnosti (RSB) na kusema ’’ linatoa huduma za kurekebisha na kudumisha utendakazi wa ndege za kijeshi’’

Libyen Symbolbild LNA
Libya inakumbwa na vita vya zaidi ya muongo mmojaPicha: Reuters/Esam Omran Al-Fetori

Lakini inasema kuwa wanaofuatilia bado wanachunguza madai kwamba mashirika mengine mawili ya makundi ya ulinzi ya Moran na Schit yamehusika .

Vikosi vinavyomuunga mkono Haftar vimekuwa vikipigana kuuteka mji mkuu wa Tripoli kutoka kwa serikali inayotambulika kimataifa ya muungano wa kitaifa –GNA-  tangu Aprili 2019

Muingilio wa jeshi la kimataifa umeongeza mzozo huo huku umoja wa mataifa ya falme za kiarabu na Urusi zikimuunga mkono Haftar na Uturuki ikiiunga mkono serikali ya GNA.

Makubaliano ya Januari yaliosimamiwa na Uturuki na Urusi yamekiukwa mara kwa mara.

Kuhusika kwa kundi la Wagner katika mzozo huo kwanza kulifichuliwa na magazeti ya The New York Times na The Washington Post mwaka jana.  Gazeti la New York Times liliweka idadi yake kuwa 200 huku la Washington Post likisema kuwa huenda idadi hiyo ikawa juu kufikia maelfu kadhaa.

Umoja wa Mataifa haupendekezi vikwazo dhidi ya makundi hayo ama hatua yoyote ya kuzuia kuhusika kwao.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, ripoti ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres iliyowasilishwa kwa baraza la kiusalama Jumanne na pia ilitaja mamluki wa kigeni lakini haikuwatambua ama kupendekeza hatua yoyote dhidi yao.

 

dpa, afp