1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukiukaji wa Haki za Binadamu nchini Urusi

P.Martin16 Julai 2007

Wagombea haki za binadamu nchini Urusi na Finland wana hofu kuwa ukiukaji wa haki utaendelea hata baada ya awamu ya Rais Vladimir Putin.Kiongozi huyo wa Urusi anatazamiwa kuondoka madarakani mwezi Machi mwaka ujao.

https://p.dw.com/p/CHkB
Kiongozi wa upinzani,Sergei Gulyayev akikamatwa na polisi wa kuzuia ghasia mjini St.Petersburg
Kiongozi wa upinzani,Sergei Gulyayev akikamatwa na polisi wa kuzuia ghasia mjini St.PetersburgPicha: AP

Kwa maoni ya Naibu-Profesa Dmitry Lanko wa Chuo Kikuu cha St.Petersburg,“Mtu mpya mwenye jina jingine atachomoza,lakini atakuwa Putin mpya.“

Lanko alikuwa akizungumza kwenye semina iliyoandaliwa na Jopo la Kiraia la Finland na Urusi kama sehemu ya kampeni ya kuyaunga mkono makundi ya kiraia nchini Urusi yanayopigania haki za kiraia na uhuru wa kisiasa.

Wakati huo huo mbunge wa Finland Heidi Hautala alie mwenyekiti wa jopo hilo amesema,kile kinachochukuliwa kama ni jambo la kawaida nchini Finland kama vile kuunda shirika lisilo la kiserikali,si jambo la kawaida nchini Urusi. Sababu ni kwamba watu wanaohusika na harakati za aina hiyo,wanaweza kushtakiwa kuambatana na sheria ya Urusi kwamba wanahusika na siasa kali.

Baada ya iliyokuwa Soviet Union kusambaratika mwanzoni mwa miaka ya tisini,kulikuwepo matumaini makubwa kuwa Urusi yenye udemokrasia zaidi, itachukua nafasi ya mfumo wa kiimla wa Soviet Union ya zamani.Lakini matumaini hayo yamevunjika tangu Putin kushika madaraka takriban miaka minane iliyopita.

Kwa maoni ya Lyudmila Alekseyev,ambae ni mwanaharakati wa Kirusi anaegombea haki za binadamu tangu enzi ya Kisoviet,haitoshi tu kupigania haki za binadamu.Njia pekee ya kuhakikisha mustakabali ni kujenga jamii ya kiraia iliyo imara nchini Urusi-jamii itakayoweza kusimama kidete mbele ya urasimu na ukiritimba wa kikundi cha watu wachache.

Akaongezea kuwa huenda ikachukua hadi miaka 15 kabla ya kuweza kuvuna matunda ya juhudi hizo.

Hivi sasa nchini Urusi,takriban vituo vyote vikuu vya televisheni vinadhibitiwa na serikali,kwa hivyo nafasi ya kusikia sauti za upinzani ni ndogo mno.

Wanaharakati wanaogombea haki za binadamu wanasema,waandishi wa habari wanaopaza sauti dhidi ya ulaji rushwa na ukiukaji wa haki za binadamu,wanakabiliwa na hatari kubwa ya kufungwa jela au kitisho cha kifo.

Kwa mfano,inaaminiwa kuwa ile kesi ya mauaji ya muandishi wa habari wa Kirusi,Anna Politkovskaya, hapo Oktoba mwaka jana,inahusika na ukosoaji wa mara kwa mara wa muandishi huyo wa habari.Yeye ameituhumu Urusi ukiukaji wa haki za binadamu katika vita vya Chechnya.Kesi hiyo,iligonga vichwa vya habari na ililaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa.

Lanko anaeleza kuwa uongozi wa sasa nchini Urusi, upo katika mikoni ya watu walio wafanya biashara kuliko wanasiasa.Anasema,si siri kuwa Rais Putin ana maslahi makubwa katika shirika la Gazprom ambalo ni shirika kubwa kabisa la mafuta na gesi nchini Urusi na sehemu kubwa ya hisa za shirika hilo,hudhibitiwa na serikali.Vile vile vongozi wengine wa tabaka ya juu,ni wakurugenzi watendaji wakuu wa mashirika makubwa.Kwa maoni ya Lanko, watu hao hawapo tayari kuachana na hayo yote kwa hiyari.