1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yazindua mkakati mpya wa kuamiliana na China

Iddi Ssessanga
13 Julai 2023

Ujerumani imetangaza waraka wa sera mpya ya kuamiliana na China inayozidi kujitanua, baada ya miezi kadhaa ya mjadala mkali kuhusu mkakati madhubuti kuelekea mshirika huyo mkuu wa kibiashara wa Berlin.

https://p.dw.com/p/4TrOe
Belgien Brüssel | Außenministerin Annalena Baerbock gibt Pressestatement vor Sitzung
Picha: Thomas Koehler/photothek/picture alliance

Ukilenga kuweka uwiano kati ya maslahi kinzani ya taifa lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, waraka huo unaainisha mabadiliko makubwa katika msimamo wa Ujerumani kuelekea China kama mshirika, mshindani na mpinzani wa kimfumo.

Waraka huo wenye kurasa 64, ambao serikali inasema ni sehemu muhimu ya mkakati wa Umoja wa Ulaya kuelekea China, unalenga kuwa halisi lakini siyo ujinga, kulingana na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock. Waraka huo ni matokeo ya miezi kadhaa ya malumbambano ndani ya serikali ya Ujerumani kuhusiana na mkakati wake kuelekea China.

Wakati Baerbock, mwanasiasa kutoka chama mshirika katika serikali ya mseto cha Watetezi wa Mazingira, ameshinikiza msimamo mkali zaidi na msisitizo juu ya haki za binadamu, Kansela Olaf Scholz, Msosho Demokrat, ameunga mkono msimamo ambao ni rafiki zaidi kwa biashara.

Deutschland | Vorstellung des Koalitionsvertrags
Viongozi wakuu katika serikali ya muungano ya Ujerumani, kutoka kushoto: Christian Linder, waziri wa fedha na mkuu wa chama cha FDP, Olaf Scholz, kansela wa Ujerumani kutoka chama cha SPD, Annalena Baerbock, mwenyekiti mwenza wa chama cha Kijani na waziri wa mambo ya nje, na Robert Habeck, mwenyekiti mwenza wa chama cha Kijani, ambayni ni naibu kansela na waziri wa uchumi.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Muungano wa Scholz wa vyama vitatu ulikuwa umeahidi baada ya kuingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2021, kuunda "mkakati mpaka wa China." Ujerumani ndiyo yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya na ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu katika umoja wa Ulaya.

Soma pia: Ujerumani, China zafanya mazungumzo ya ngazi ya juu

Mkakati wake unalenga kuweka usawa: Unataka kubakisha uhusiano mzuri na China, ambyo ndiyo mshirika wake mkubwa zaidi wa kibiashara katika miaka ya karibuni, licha ya wasiwasi kuhusiana na ubabe unaozidi wa China na kukataa kukosoa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Sera hiyo inaashiria usawa uliosawazishwa vizuri kati ya Baerbock na Scholz ndani ya muungano unaotawala, ambao ni matokeo ya kile Baerbock alichokiita "kutafuta maelewano... ambayo ndiyo msingi wa demokrasia.

Kupunguza hatari kunahitajika

Waraka huo wa kimkakati unabainisha kwamba "wakati utegemezi wa China kwa Ulaya unazidi kupungua, utegemezi wa Ujerumani kwa China umepata umuhimu mkubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Serikali ya Ujerumani imesema haikukusudia kuzuwia ukuaji na maendeleo ya kiuchumi ya China, lakini wakati huo imeongeza kuwa kuondoa hatari kunahitajika haraka.

Berlin | Deutsch-chinesische Regierungskonsultationen
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, kulia, na waziri mkuu wa China, Li Qiang, kushoto, wakizungumza na waandishi wa habari baada ya mashauriano ya mataifa mawili karika ofisi ya kansela mjini Berlin, Juni 20, 2023.Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Soma pia: China yasema Beijing inapendelea ushirikiano na Ujerumani

Berlin inafuatilia kwa wasiwasi namna China inavyojitahidi kushawishi utaratibu wa kimataifa kulingana na maslahi ya mfumo wake wa chama kimoja na hivyo kupuuza misingi ya utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria, kama vile hadhi ya haki za binadamu.

Hata hivyo Ujerumani pia imeangazia uwezekano wa ushirikiano zaidi, ikibainisha kwa mfano kwamba "haitawezekana kushinda mzozo wa tabianchi bila China".

Ikiwa na kumbukumbu mbaya ya utegemezi wake kwa nishati ya gesi kutoka Urusi na kuumizwa na uvurugaji wa mifumo ya ugavi wakati wa janga la UVIKO-19, Ujerumani imekuwa ikiongeza juhudi za kuondokana na utegemezi wa China.

Chanzo: mashirika