Ujerumani yatoa ulinzi kwa Kanisa la Coptic | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.01.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani yatoa ulinzi kwa Kanisa la Coptic

Polisi ya Ujerumani imesema inachukua hatua za kuwalinda Wakristo wa madhehebu ya Coptic watakaposherehekea sikukuu ya Krismasi, Ijumaa ijayo (7 Januari 2010) dhidi ya kitisho cha mashambulizi ya kigaidi.

Vijana wa madhehebu ya Kikristo ya Coptic wakibeba mabango yanayoilaumu serikali ya Misri kwa shambulizi la mabomu dhidi ya Kanisa lao, mjini Alexandria

Vijana wa madhehebu ya Kikristo ya Coptic wakibeba mabango yanayoilaumu serikali ya Misri kwa shambulizi la mabomu dhidi ya Kanisa lao, mjini Alexandria

Siku nne baada ya mashambulizi dhidi ya kanisa la Wakristo wa madhehebu ya Coptic huko nchini Misri, jeshi la polisi ya mjini Hannover limetoa ahadi ya kuwalinda waumini wa kanisa hilo nchini Ujerumani katika sherehe yao ya Krismasi inayofanyika Ijumaa ijayo.

Katika shambulio la mjini Alexandria nchini Misri, watu 21 waliuawa, baada ya bomu kuripuka dakika 20 tu baada ya mwaka mpya kuanza. Watu wengine 100 walijeruhiwa katika shambulio hilo.

Serikali ya Ujerumani iliungana na mataifa mengine kulaani shambulio hilo, ambapo msemaji wa serikali, Christoph Steegmans, alisema kwamba, ni jambo lisilokubalika kuwashambulia watu wasiokuwa na hatia, ambapo Waislamu pia walipoteza maisha yao.

Uamuzi wa Polisi ya Hannover kuwalinda Wakristo hao wa madhehebu ya Coptic unatokana na vitisho vilivyotolewa na magaidi dhidi yao na kuchapishwa kwenye mtandao. Polisi hiyo itakuwa macho zaidi katika siku za Alhamis na Ijumaa, ambapo sherehe za Krismasi za kanisa hilo zitafanyika.

Kwa mujibu wa takwimu, wapo Wakristo 6,000 wa madhehebu ya Coptic nchini Ujerumani. Na moja ya makanisa ya madhehebu hayo, lipo katika mji wa Hannover.

Sawa na Wakristo wengine wanaofuata imani asilia, Wakristo wa madhehebu ya Coptikc wanasherehekea Krismasi siku kadhaa baada ya Wakristo wa nchi za Magharibi.

Hatua za kulinda usalama wa Wakristo wa kanisa la Coptic zimeimarishwa katika nchi kadhaa, baada ya kundi la wanaitikadi kali, linaloitwa 'Nchi ya Kiislam ya Irak', kuchapisha majina ya watu 150 wanaokusudiwa kuuawa miongoni mwa Wakristo wa kanisa hilo.

Wizara ya Usalama ya Uholanzi imetangaza kuwa itaimarisha usalama kwenye makanisa ya Coptic katika miji ya Amsterdam, Eindhoven na Utrecht. Wakristo kwenye makanisa hayo pia wamewekwa katika orodha ya watu wanaokusudiwa kuuawa na wanaitikadi kali wa Kiislam.

Wakati huo huo, watetezi wa haki za binadamu nchini Misiri, wamesema kuwa mapungufu ya sera ya serikali katika kuishughulikia mivutano ya kidini, yamesababisha mazingira yaliyowawezesha magaidi kuwashambulia Wakristo wa Kanisa la Coptic.

Asasi 12 za watetezi wa haki za binadamu nchini humo, zimesema katika tamko kwamba, mashambulio yaliyofanywa kwenye kanisa la mjini Alexandria lazima yashughulikiwe kwa kutilia maanani kuongezeka mivutano baina ya jamii za kidini nchini Misri.

Mwandishi: Abdu Mtullya/AFP/ZAR

 • Tarehe 04.01.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/ztaJ
 • Tarehe 04.01.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/ztaJ

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com