1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatamba tena Uturuki

Sekione Kitojo8 Oktoba 2011

Ujerumani imeendeleza rekodi ya kushinda michezo yake katika kundi A, wakati ilipofanikiwa kuiangusha Uturuki mbele ya mashabiki wake mjini Istanbul, Uturuki kwa mabao 3-1.

https://p.dw.com/p/12o72
Hiki ndio kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani , ambacho kiliisambaratisha UturukiPicha: picture alliance/Pressefoto Ulmer

Yaliyojiri viwanjani zaidi ni kuhusu michezo iliyofanyika jioni ya jana katika bara la Ulaya, ikiwa timu za taifa katika bara hili zilikuwa zinawania kukata tikiti katika fainali za kombe la mataifa ya Ulaya , Euro 2012. Na Ujerumani ambayo tayari ilikuwa imekwisha kata tikiti yake , ilipambana jana na Uturuki ambayo ilikuwa nyumbani kuwania points tatu muhimu ambazo zingeiweka nchi hiyo katika nafasi ya kukata tikiti yake katika kinyang'anyiro hicho. Ujerumani imeendeleza ubabe wake katika kundi A, baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 mjini Istanbul Ijumaa jioni.

Ushindi huo , ambao umepatikana kupitia magoli ya Mario Gomez, Thomas Mueller na Bastian Schweinsteiger, umeiweka Ujerumani katika points 27 kutokana na michezo tisa , wakati Uturuki imeporomoka hadi nafasi ya tatu ikiwa na points 14, moja nyuma ya Ubelgiji , ambayo nayo iliiangusha Kazakhstan na inakabiliana na Ujerumani katika mchezo wao wa mwisho siku ya Jumanne.

Kocha wa Ujerumani Joachim Löw, ambaye aliuanza mchezo huo na wachezaji saba wa viongozi wa ligi ya Ujerumani Bundesliga , Bayern Munich , amesema kuwa timu yake imefanya kile ambacho ilistahili kufanya.

Fußball EM-Qualifikation 2011 Deutschland gegen Türkei
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew .Picha: dapd

Sina budi kuwapongeza wachezaji wangu, amesema Löw. Wamefanya vizuri dhidi ya timu ambayo ilikuwa inalazima ya kushinda na kupewa nguvu na mashabiki wake wa nyumbani.

Ushindi huo unaifanya Ujerumani kuvunja rekodi yake ya ushindi wa mfululizo katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza katika fainali. Rekodi yake bora ilikuwa katika michuano ya mtoano kwa ajili ya fainali za kombe la dunia mwaka 1982, wakati Ujerumani iliposhinda michezo yake nane ya mwanzo. Mlinda mlango wa Ujerumani Manuel Neuer amesema kuwa wachezaji walihitaji kushinda mchezo huo wakati wakitafuta kushinda mara ya kumi kutokana na michezo kumi. Kwa hilo tulihitaji kushinda dhidi ya Uturuki na sasa lengo ni kushinda katika mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Ubelgiji.

Wakati huo huo mabingwa wa Ulaya Hispania wamekata matumaini ya jamhuri ya Chek ya kupata nafasi ya pili katika kundi I kwa ushindi bila jasho wa mabao 2-0 kutokana na magoli yaliyowekwa wavuni na Juan Mata nma Xabi Alonso.

Ushindi huo wa Hispania , ambayo imepata points zote 21 kutoka michezo yake saba na tayari imeshafuzu kucheza katika fainali, umeiacha jamhuri ya Chek points mbili mbele ya Scotland. hata hivyo timu hiyo imecheza mchezo mmoja zaidi, na wanatumai kuwa Wascoch, ambao wanazuru Liechtenstein leo na Hispania Jumanne ijayo , wanapoteza points.

Mshambuliaji nyota wa uingereza Wayne Rooney alionyeshwa kadi nyekundu licha ya Uingereza kufanikiwa kufuzu kuingia katika fainali za euro 2012. Rooney alikandikwa kadi nyekundu katika dakika ya 73 mjini Podgorica wakati Montenegro ilipopambana kutoka kuwa chini kwa mabao 2-0 na kurejesha mabao hayo na kulazimisha sare ya mabao 2-2.

Fußball Bayern München Manchester United April 2010
Wayne Rooney wa Uingereza alitolewa nje kwa kadi nyekundu dhidi ya Montenegro.Picha: AP

Kocha wa Uingereza Fabio Capello ana matumaini kuwa Rooney atajifunza kutokana na makosa yake licha ya kuwa mchezaji huyo atakosa mchezo ujao pamoja na huenda mchezo mmoja wa fainali hizo.

Ufaransa iliisambaratisha Albania kwa mabao 3-0 mjini Paris ikibakiza point moja kabla ya kufuzu kuingia katika fainali hizo. Nimeridhika, amesema kocha wa Ufaransa Laurent Blanc, tulitaka kushinda mchezo huu na kila mara inakuwa ni jambo la kufurahisha iwapo nia hiyo inatimia. Ureno nayo iliirarua Iceland kwa mabao 5-3, ambapo mshambuliaji wa Manchester United Nani alipachika mabao mawili. Hayo ni baadhi ya yale yaliyojiri katika vieanja vya michezo Mayram.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae