1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yarefusha ujumbe wa Afghanistan

P.Martin12 Oktoba 2007

Bunge la Ujerumani hii leo,limepiga kura kubakisha vikosi vyake nchini Afghanistan kwa mwaka mmoja mwingine,kinyume na maoni ya umma unaopinga vikali ujumbe huo.

https://p.dw.com/p/C7hq

Bunge la Ujerumani-Bundestag limekubali kurefusha ujumbe wa wanajeshi 3,500 kama sehemu ya kikosi cha kimataifa cha ISAF kinachoongzwa na NATO kulinda usalama nchini Afghanistan.Bunge hilo pia limetoa idhini ya kurefusha muda wa kutumia ndege zake sita za upelelezi,aina ya Tornado.

Ujumbe huo,umezusha mabishano makali Ujerumani- nchi ambayo tangu kumalizika Vita Vikuu vya Pili, ndio kwanza imeanza kushiriki katika tume za kijeshi kwenye nchi za ngámbo.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani,Franz Josef Jung ameutetea ujumbe huo sawa na waziri wa maendeleo wa Ujerumani,Bibi Heidemarie Wiezcorek Zeul alietangaza kuwa msaada wa kutoa mafunzo kwa vikosi vya polisi na kuanzisha mahakama, utaimarishwa sawa na msaada wa fedha kwa ajili ya miradi ya kiraia,nchini Afghanistan.

Lakini upinzani wa umma nchini Ujerumani umeongezeka,baada ya wanajeshi 26 wa Kijerumani kuuawa nchini Afghanistan.Uchunguzi wa maoni ya umma uliofanywa na gazeti la Kölner Stadt Anzeiger umeonyesha kuwa ni asilimia 29 tu huunga mkono kurefusha ujumbe wa Ujerumani nchini Afghanistan.

Juu ya hivyo,hii leo wabunge 454 wameunga mkono kurefusha ujumbe huo;79 walipinga na wengine 48 walizuia kura zao.

Vikosi vya Ujerumani,hasa vipo kaskazini mwa Afghanistan na katika mji mkuu Kabul.Serikali ya Berlin imepinga mwito wa NATO,kusaidia kutoa mafunzo kwa vikosi vya Afghanistan katika eneo la hatari zaidi,kusini mwa nchi ambako vikosi vya NATO vinakabiliwa na uasi mkali kutoka wanamgambo wa Kitaliban.

Juma hili,waasi wa Kitaliban walimuachilia huru mateka wa Kijerumani aliezuiliwa kwa takriban miezi mitatu.Mwenzake alietekwa nyara wakati huo huo,ameuawa.Wataliban,walidai kuwa Ujerumani iondoshe vikosi vyake kutoka Afghanistan,lakini Berlin ilikataa kuitikia dai hilo.

Mwaka huu peke yake,wanamgambo wa Kitaliban wamefanya zaidi ya mashambulizi 100 ya kujitolea muhanga.Sasa nchi kama Uholanzi na Kanada zinazidi kushinikizwa na umma kupunguza idadi ya wanajeshi wake au zitangaze tarehe ya kuvirejesha nyumbani vikosi hivyo.