Ujerumani yaibuka kidedea tiketi ya Euro 2012 | Michezo | DW | 12.10.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Ujerumani yaibuka kidedea tiketi ya Euro 2012

Katika mpambano wa jana jioni (11.10.2011) kuwania tiketi ya Kombe la UEFA 2012, timu ya taifa ya Ujerumani imemaliza vyema mzunguko wake wa Kundi A, baada ya kuibwaga Ubelgiji kwa mabao 3-1.

Mesut Oezil wa Ujerumani akishangilia bao la ushindi dhidi ya Ubelgiji. ,

Mesut Oezil wa Ujerumani akishangilia bao la ushindi dhidi ya Ubelgiji. ,

Mesut Oezil, Andre Schuerrle na Mario Gomez, ndio waliolazimisha Ubelgiji kutoka uwanjani kichwa chini.

"Tulitaka kushinda mchezo huu wa mwisho kwa namna yoyote ile. Tulianza taratibu, lakini baada ya goli la kwanza tulionesha kile tunachoweza kukifanya." Amesema Mesut.

Ujerumani imemaliza ikiwa nafasi ya juu kabisa kwenye kundi A, ikiwa na pointi 30 na magoli 34-7. Ubelgiji, iliyofungwa na Ujerumani, imekosa nafasi ya mchezo wa marudio, kwa kuwa na pointi 15, baada ya Uturuki kuifunga Azerbaijan 1-0, na hivyo kumaliza ya pili kwenye kundi A, ikiwa na pointi 17.

Nako jijini Paris, mabingwa mara mbili wa kombe hili, Ufaransa, waliokolewa na na mkwaju wa penalti wa Samir Nasri katika dakika za majeruhi, ambayo iliyafanya matokeo ya mechi yake na Bosnia-Herzegovina kuwa suluhu ya 1-1.

Mapema katika dakika ya 40, goli la Edin Dzeko lilikuwa limeshawaweka Wabosnia kwenye nafasi ya juu kwenye kundi D. Penalti ya Nasri, anayechezea Manchester City ya Uingereza, katika dakika ya 78, iliifanya Ufaransa kumaliza mchezo huo ikiwa na pointi 21 dhidi ya 20 za Bosnia-Herzegovina.

Sasa Ufaransa, Hispania, Sweden, Denmark na Urusi zimefanikiwa kujiunga na Ujerumani, Italia, Uingereza na Uholanzi kwenye fainali za kombe la Euro 2012, ambalo mwaka huu zinafanyika nchini Ukraine na Poland kwa pamoja.

Ireland, Uturuki, Bosnia-Herzegovina, Croatia, Ureno, Montenegro, Jamhuri ya Czech na Estonia zilimaliza katika nafasi ya pili kwenye makundi yao na mechi za kuwapata washiriki wanne miongoni mwao zitafayika mwezi ujao.

Bahati mbaya, hata hivyo, iko kwa mchezaji bora wa zamani wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, ambaye huenda asishiriki fainali za mara hii, kwa kuwa timu yake ya taifa ya Ureno, imetolewa na Denmark katika kundi H kwa mabao mawili kwa moja.

Magoli ya Michael Krohn-Delhi katika dakika ya 13 na Nicklas Bendtner katika dakika ya 63 ndiyo yaliyozizamisha ndoto za Ureno. Denmark imefanikiwa kumaliza ikiwa na pointi 19, zikiwa ni tatu zaidi mbele ya Ureno.

Uwanja wa Olimpiki wa Kiev, Ukraine, kutakakochezwa mechi za Euro 2012.

Uwanja wa Olimpiki wa Kiev, Ukraine, kutakakochezwa mechi za Euro 2012.

Ushindi wa 2-1 wa Sweden dhidi ya Uholanzi, umeipandisha Sweden moja kwa moja katika nafasi ya pili kwenye kundi E, huku Uholanzi ikisalia na nafasi yake ya kwanza kwenye kundi hilo. Uholanzi inaongoza kundi E kwa kuwa na pointi 27, huku Sweden ikiwa na pointi 24. Sasa zote mbili zinaingia kwenye Kombe la Euro 2012.

Hispania, ambayo mwaka 2008 iliilaza Ujerumani kwenye fainali za kombe la Ulaya, nayo imemaliza mzunguko wake wa kundi I kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Scotland. David Silva aliweka kimiani mabao mawili kati ya hayo na David Villa akaipandisha juu rekodi yake ya kufunga bao la 50 kwenye mechi za kimataifa. Waczech wamemaliza katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 13, baada ya ushindi wao wa 4-1 dhidi ya Lithuania.

Magoli yaliyofungwa na Giorgos Fotakis na Angelos Charisteas wa Ugiriki katika dakika za 79 na 85 yalilipiku bao moja la Georgia lililowekwa kimiani na David Targamadze. Kwa matokeo hayo, Ugiriki ambao walichukuwa Kombe la Europa mwaka 2004, wameamaliza mzunguko wakiwa wanaongoza kwenye Kundi F na wakiwa na pointi 24.

Croatia ilimaliza kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Latvia, yaliyofungwa kwenye kipindi cha pili. Mabao hayo ya Eduardo na Mario Mandzukic yanaifanya Croatia kumaliza ikiwa ya pili kwenye F ikiwa na pointi 22.

Lakini ushindi wa kusisimua kuliko wote hapo jana jioni, umekuwa ni ule wa Urusi dhidi ya Andorra. Urusi iliibwaga timu hiyo ya taifa dogo lenye raia 85,000 tu, kwa mabao 6-0 na kuifanya iongoze kundi B ikiwa na pointi 23.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA
Mhariri: Josephat Charo