1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNHCR: Suala la wakimbizi ni la Ulaya nzima

18 Agosti 2015

Mkuu wa shirika la kuwashughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa ameonya leo kuwa Ujerumani na Sweden haziwezi kuachwa kubeba peke yao mzigo wa ongezeko la waomba hifadhi barani Ulaya

https://p.dw.com/p/1GHKD
Kos Küste Strandpromenade Flüchtlinge Zelte
Picha: picture-alliance/dpa/Odysseus

Hayo ni wakati vyombo vya habari vya Ujerumani vikiripoti kuwa idadi ya watu wanaotafuta hifadhi katika nchi hiyo huenda ikaongezeka hadi 750,000 mwaka huu.

Katika mahojiano yaliyochapishwa na gazeti la Die Welt, Mkuu wa Shirika la Kuwashughulikia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa – UNHCR Antonio Guterres ametoa wito wa kuwapo mshikamano zaidi miongoni mwa mataifa ya Ulaya katika kuwapa hifadhi wato wanaokimbia vita na mateso katika nchi zao.

Ujerumani, kama taifa kubwa lenye nguvu za kiuchumi barani Ulaya, imekuwa kituo kikuu cha kuwakaribisha wakimbizi. Mmoja kati ya watu watatu waliowasili mwaka jana katika Umoja wa Ulaya waliomba hifadhi nchini Ujerumani.

Serikali ya Ujerumani ilitabiri kuwa idadi ya wakimbizi ingefikia 500,000 mwaka huu lakini gazeti la Handelsblatt limenukuu duru za serikali leo zikisema kuwa idadi hiyo huenda ikapanda hadi 750,000.

Griechenland Flüchtlinge Lesbos
Wakimbizi wanaendelea kuwasili katika fukwe za UgirikiPicha: Getty Images/AFP/A. Zavallis

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema leo kuwa Ugiriki ni lazima ionyeshe “uongozi zaidi” ili kukabiliana na mgogoro unaoongezeka ambapo wakimbizi na wahamiaji 160,000 wamesili katika fukwe zake kufikia sasa mwaka huu.

Msemaji wa UNHCR William Spindler amesema mjini Geveva kuwa serikali ya Alexis Tsipras inakabiliwa na mgogoro wa kifedha lakini ina wajibu wa kuchukua hatua, na Umoja wa Ulaya lazima uisaidie Ugiriki. "ikiwa serikali kuu ya Ugiriki itaweka uongozi imara na kumteua mtu ambaye anaweza kusimamia suala la wakimbizi basi sisi na mashirika mengine ya kimataifa tutakuwa tayari kuja na kusiadia. Lakini ni vigumu kwetu, kuanza kufanya kazi nchini humo ikiwa hatuma mtu anayesimamia shughuli hizo2.

Ujerumani itachapisha kesho takwimu mpya, na ikiwa makadirio hayo yatathibitishwa, itakuwa rekodi mpya na mbali kabisa na ile ya awali ya juu mnamo mwaka wa 1992, wakati Ujerumani ilipofungua milango yake kwa wakimbizi waliokuwa wakikimbia vita vya mataifa ya Balkan.

Ongezeko hilo kubwa la idadi ya wakimbizi limeiacha Ujerumani ikijitahidi kutafuta mbinu za kuwapa hifadhi wakimbizi huku mahema na shule zikitumika kama makaazi ya muda.

Mamlaka za majimbo zimekuwa zikitoa wito wa kutolewa msaada zaidi wa serikali kuu ili kusaidia kuikabili hali hiyo. Kansela wa Ujerumani ameonya kuwa mgogoro wa waomba hifadhi unatishia kuwa changamoto kubwa zaidi kwa Ulaya kuliko matatizo ya madeni ya Ugiriki.

Katika Umoja wa Ulaya, Sweden ilisajili idadi kubwa ya waomba hifadhi katia mwaka wa 2014 – asilimia 13, ijapokuwa ukilinganisha na idadi ya watu wake, nchi hiyo ndiyo inayoubeba mzigo mkubwa zaidi katika umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri:Josephat Charo