Ujerumani kuitambua Sudan ya Kusini haraka
16 Juni 2011Msemaji wa serikali ameeleza kuwa Ujerumani itaanzisha uhusiano wa kibalozi na nchi hiyo baada ya uhuru kutangazwa na itafungua ofisi ya ubalozi katika mji mkuu Juba.
Kwa kuitambua Sudan ya Kusini haraka,Ujerumani na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya zinakusudia kutoa mchango katika kuleta utengemavu kwenye eneo lote linalopakana na Sudan. Hivi karibuni watu wa jimbo la Sudan ya Kusini walipiga kura ya maoni na kuamua kujitenga na Sudan ya Kaskazini.
Ujerumani imefahamisha juu ya hatua ya kuitambua Sudan ya Kusini muda mfupi tu baada ya kuzindua sera mpya juu ya Afrika inayoweka mkazo katika kukidhi maslahi ya Ujerumani, badala ya kutoa hisani ya msaada wa maendeleo kwa bara hilo. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle aliitangaza sera hiyo kabla ya kuanza ziara nchini Sudan iliyoahirishwa baadae kutokana na mripuko wa jivu la moto nchini Eritrea .
Kwa mujibu wa sera hiyo mpya wafanya biashara wa Ujerumani watahimizwa kufikia mapatano yatakayojumuisha malengo ya kuweka vitega uchumi na kupatiwa haki za uziduaji wa madini.