Ujerumani katika Kombe la dunia kundi D | Michezo | DW | 09.06.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Ujerumani katika Kombe la dunia kundi D

Je, Ghana itaitilia Ujerumani kitumbua chake mchanga ?

default

Nahodha mpya:philipp Lahm

Ujerumani ,ina sifa ya kuvaa taji la Kombe la dunia mara 3-1954 mjini berne,Uswis ilipoilaza Hungary ,1974 nyumbani ilipoitoa Holland na 1990 nchini Itali ilipoivua taji Argentina.Mara hii lakini kikosi cha Joachim Löw,hakitapata mteremko dhidi ya Kangaroo-Australia,Black Stars Ghana na Serbia -timu za kundi D.

Ujerumani bila ya nahodha wake Michael Ballack itakuwa uwanjani kwa mara ya kwanza Jumapili hii ikiwa na miadi na Australia.

Kwa kuwasili finali ya kombe la Ulaya 2008 na kupokonywa Kombe na Spain,kwa sehemu kubwa timu chipukizi ya Ujerumani,haikujaribiwa barabara kuhimili zahama za Kombe la dunia.Hatahivyo, itateremka uwanjani Jumapili hii na chipukizi wengi waliopania kujaza pengo la akina Ballack na Oliver Kahn.

Isitoshe, licha ya misukosuko yake mingi ilioikumba Ujerumani kuanzia kuumia kwa kipa wake Rene Adler, hadi nahodha wake Michael Ballack,Ujerumani ina sifa ya kutamba inapojikuta kwenye misukosuko na ikivukaq salama usalimini duru ya kwanza,basi gari-moshi la Ujerumani, ni vigumu kulizuwia lisiwasili finali hapo Julai 11,City Stadium,Johannesberg. Kumbuka pia Ujerumani, imeshinda changamoto zote 4 za mikwaju ya penalty katika vikombe vilivyopita vya dunia.Inaelewa jinsi ya kuvumilia vishindo na kumtuliza shetani.

Hatahivyo, kocha Joachim Löw,hataiachia bahati nasibu kuamua.Amejiandaa barabara na chipukizi wake wanaojumuisha Podolski,Mueller,Kiessling na Mbrazil,Cacau aliechukua uraia wa Ujerumani.

Chipukizi mwengine, ni kipa Manuel Neuer,atakae kuwa na kibarua kizito cha kujaza pengo la Oliver Kahn,aliestaafu.

Katika kundi hili D, Serbia, ilitamba katika kinyan'ganyiro cha kuania tikieti za Kombe la dunia-kanda ya ulaya.Kwahivyo, Ujerumani, itabidi kuchunga.

"Itakuwa pia kibarua kigumu kuitimua nje Black Stars-Ghana,kutokana na nguvu zao za kimwili."

Alisema kocha Löw.

Ghana, kwa kuwa timu pekee ya Afrika kuwasili duru ya pili ya Kombe lililopita la dunia hapa Ujerumani, Ujerumani, inaamini kuwa Ghana, ndie itakayoipa mtihani mkubwa katika kundi hili D.Na hii licha ya kuumia kwa stadi wao Michael Essien.

Chini ya usukani wa kocha wao Mserbia,Milovan Rajaevac,Ghana, ilikata tiketi yake ya Kombe la dunia bila ya shida.Ni Ghana iliocheza finali ya Africa Cup na Misri, huko Angola.

Hatahivyo, matatizo yamechomoza katika kikosi cha Black Stars,tangu kuumia kwa Essien na kocha Rajevac, anasubiri kwa hamu kuu kujua iwapo Sulley Muntari, wa Inter Milan,atapona mapema ili kujiunga nao kwa mpambano wa Jumapili hii na Serbia.Maarifa ya nahodha Stephen Appiah, huenda yakawasaidia sana Black Stars ili nyota yao-nyeusi inawiri katika mawingu ya Afrika Kusini.Pigo walilopata majuzi la mabao 4-1 kutoka Holland, si dalili njema hatahivyo.Kocha wao Rajaevac, anasema anaiheshimu sana Ujerumani,lakini, anaamini Ghana, yaweza kuitilia Ujerumani kitumbua chake mchanga,hapo Juni 23 na kutoroka na tiketi ya duru ya pili ya kutoana kama katika kombe lililopita la dunia 2006,hapa Ujerumani.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ AFPE

Uhariri: Aboubakary Liongo

 • Tarehe 09.06.2010
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/NmDm
 • Tarehe 09.06.2010
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/NmDm